Habari
SERIKALI KUREJESHA KWA KIWANDA CHA CHAI LUPEMBE
Serikali imetangaza kuwa mchakato wa kurejesha Kiwanda cha Chai cha Lupembe (MUVYULU) kilichopo mkoani Njombe umefikia hatua nzuri, kufuatia makubaliano ya hivi karibuni ya kumaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya mwekezaji na wakulima.
Hayo yameelezwa Aprili 20, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo(Mb), kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), wakati akijibu swali namba 142 la Mbunge wa Lupembe, Mhe. Edwin Swalle, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itarejesha kiwanda hicho kwa wakulima wa Lupembe.
Amebainisha kuwa kiwanda hicho kilibinafsishwa mwaka 2004 kwa Kampuni ya Dhow Mercantile Ltd (DML), ambapo kampuni hiyo ilipewa asilimia 70 ya hisa na asilimia 30 kubaki kwa Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Chai (MUVYULU). Hata hivyo, baada ya ubinafsishaji huo, kulizuka mgogoro wa uendeshaji na umiliki uliopelekea suala hilo kufikishwa mahakamani.
Aidha, amebainisha kuwa, kupitia usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), pande zote mbili zilikubali kumaliza mgogoro huo nje ya mahakama, na Kikao cha mwisho cha maridhiano kilifanyika tarehe 13 Machi, 2026, kikishirikisha wadau mbalimbali wakiwemo: Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara.
Bodi ya Chai na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Njombe (Njombe DC), Mwekezaji (DML) na Uongozi wa MUVYULU AMCOS.
Amesema ili kukamilisha zoezi la kurejesha kiwanda hicho, Serikali inafanyia kazi, Kukamilisha malipo ya kiasi cha Dola za Kimarekani 322,000 kwa Kampuni ya Dhow Mercantile Ltd kama fidia ya uwekezaji wao, Kukamilisha zoezi la uthamini wa kiwanda ili kujua thamani halisi ya mali zilizopo.
Hatua hii ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha viwanda vilivyokuwa na migogoro vinafufuliwa na kutoa tija kwa wananchi na uchumi wa Taifa.
