Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MIFUMO YA KODI NA TOZO


Serikali kuendelea kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara nchini, ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa kodi na tozo, kwa kujiweka kama wawezeshaji wa sekta binafsi badala ya kuwa wadhibiti pekee.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), Agosti 12, 2026 kwenye mkutano na wafanyabiashara wa Mkoa wa Mtwara, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani humo.


Waziri Kapinga amesisitiza kuwa zama za viongozi kuwasikiliza wafanyabiashara bila kutoa majibu au mrejesho wa kero zao zimepitwa na wakati, na sasa viongozi wana wajibu wa kisheria na kiutendaji wa kutoa majibu ya haraka.

“Tumeshasema kuwa takribani asilimia 70 ya maendeleo ya nchi yetu yanategemea sekta binafsi. Lengo letu ni kuhakikisha tunakuwa na taasisi na Sera zinazowezesha sekta hii kukua na siyo kuikandamiza,” amesema Waziri Kapinga.

Ameongeza kuwa kazi kuu ya Serikali ni kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara, huku akiwataka wafanyabiashara nao kutimiza wajibu wao kikamilifu kama ambavyo Serikali inatekeleza majukumu yake.

Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga ametoa onyo kwa mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuhujumu Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, akieleza kuwa mfumo huo una faida kubwa kwa wakulima pamoja na Serikali na umewekewa msisitizo mkubwa ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kuhusu maendeleo ya viwanda mkoani Mtwara, Mhe. Kapinga ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye miundombinu mbalimbali na hivi karibuni wananchi na wawekezaji wataanza kushuhudia mabadiliko na maendeleo makubwa katika sekta ya viwanda mkoani humo.