Habari
SERIKALI KUENDELEA KUDHIBITI UINGIZWAJI WA BIDHAA DUNI NCHINI
📌 Bidhaa zisizokidhi viwango vya Usalama vya TBS kurejeshwa zilipotoka kwa gharama ya muagizaji.
📌 Serikali yaimarisha ukaguzi wa bidhaa kabla ya kusafirishwa, zinapowasili nchini na katika masoko ya ndani.
Dodoma
Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imeimarisha mikakati ya kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zisizokidhi viwango nchini, hususan vifaa vilivyotumika (used) ambavyo havikidhi matakwa ya ubora na usalama.
Hayo yamebainishwa Oktoba 27, 2026, Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Asya Sharif Omar, aliyetaka kujua mikakati ya Serikali katika kudhibiti uingizwaji wa vifaa chakavu nchini.
Akifafanua mikakati hiyo, Mhe. Londo amesema udhibiti wa bidhaa unafanyika kupitia mifumo miwili mikuu, ambayo ni ukaguzi kabla ya bidhaa kusafirishwa kutoka nchi zinakotoka na ukaguzi zinapowasili nchini, ili kubaini bidhaa zisizokidhi viwango vinavyotakiwa.
Amesema bidhaa zitakazobainika kukiuka viwango na matakwa ya usalama zitarejeshwa katika nchi zilipotoka au kuteketezwa kwa gharama za mwagizaji, kwa mujibu wa taratibu zinazotumika.
Aidha, Mhe. Londo amesisitiza kuwa TBS inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika masoko ya ndani ili kuhakikisha bidhaa zinazouzwa na kutumiwa na wananchi zinakidhi viwango vinavyotakiwa, kwa lengo la kulinda afya, usalama na maslahi ya watumiaji.
