Habari
TANZANIA NA ZAMBIA ZAAZIMIA KUIMARISHA USHIRIKIANO KUTATUA VIKWAZO 13 VYA BIASHARA
📌 Changamoto za ucheleweshaji wa mizigo, gharama za usafirishaji na uratibu wa taasisi za mipakani zajadiliwa.
📌 Nchi hizo zakubaliana kuchukua hatua za pamoja kutatua vikwazo vilivyosalia ili kurahisisha biashara.
📌 Taarifa rasmi ya kikao yapitishwa baada ya kufanyiwa marekebisho madogo.
TUNDUMA, SONGWE.
Serikali za Tanzania na Zambia zimeazimia kuimarisha ushirikiano katika kutatua Vikwazo Visivyo vya Kikodi (Non-Tariff Barriers – NTBs) vinavyoathiri biashara baina ya nchi hizo. Azimio hilo limefikiwa katika kikao cha pamoja cha siku mbili kilichofanyika tarehe 4 na 5 Novemba 2026, katika Kituo cha Pamoja cha Huduma za Mipakani cha Tunduma (Tunduma One Stop Border Post – OSBP), mkoani Songwe.
Kikao hicho kimeratibiwa na Taasisi ya Kikanda ya Uwezeshaji Usafirishaji Ukanda wa Kati (Central Corridor Transit Transport Facilitation Agency – CCTTFA), kwa kushirikiana na taasisi husika za Tanzania na Zambia.
Kikao kimeongozwa na Bw. Ombeni Mwasha, Mkurugenzi wa Idara ya Mtangamano wa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara ya Tanzania, kwa kushirikiana na Dkt. Simon Ng’ona, Mkurugenzi wa Biashara za Nje kutoka Wizara ya Biashara na Mauzo ya Nje ya Zambia.
Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kupitia hatua zilizofikiwa katika kutatua vikwazo vilivyobainishwa awali, kujadili changamoto mpya na kuweka mapendekezo ya kuboresha biashara na usafirishaji wa bidhaa baina ya Tanzania na Zambia.
Katika majadiliano hayo, wadau wa sekta binafsi pamoja na wawakilishi wa sekta ya usafirishaji na uondoshaji mizigo wamebainisha changamoto mbalimbali zinazoathiri biashara katika njia ya Tanzania na Zambia. Changamoto hizo ni pamoja na ucheleweshaji wa magari na mizigo katika taratibu za forodha, gharama za ushuru wa barabara na tozo za halmashauri, changamoto za mizani ya magari, upungufu wa maeneo ya maegesho ya malori, pamoja na ucheleweshaji wa vibali na mawasiliano ya mifumo ya forodha kati ya nchi hizo.
Aidha, wadau wameeleza changamoto zinazohusiana na usalama wa mizigo njiani, gharama za makontena, adhabu za kuchelewa kutoka katika maeneo ya huduma pamoja na uratibu wa taasisi za mipakani.
Pia, wadau wamependekeza kuboresha mifumo ya uondoshaji mizigo kabla ya kuwasili, kuimarisha usalama wa usafirishaji, kuongeza ufanisi wa maeneo ya maegesho ya malori na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za forodha za Tanzania na Zambia.
Majadiliano hayo yalijikita pia katika vikwazo 13 ambavyo bado havijapatiwa ufumbuzi kati ya vikwazo 20 vilivyoainishwa katika kikao cha tano cha Kamati ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Zambia kilichofanyika Mei 2026. Kati ya vikwazo hivyo, saba vilikuwa vimetatuliwa huku 13 vikiendelea kuhitaji hatua za pamoja kutoka kwa taasisi husika za nchi hizo mbili.
Miongoni mwa maazimio ya kikao hicho ni kuendeleza ushirikiano wa Tanzania na Zambia katika kushughulikia vikwazo 13 vilivyosalia, kuimarisha uratibu baina ya taasisi zinazohusika na biashara na huduma za mipakani, pamoja na kuendeleza juhudi za pamoja za kuboresha uwezeshaji biashara na ufanisi wa usafirishaji wa mizigo. Aidha, wajumbe wamepitisha taarifa rasmi ya kikao hicho baada ya kufanyiwa marekebisho madogo.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Ombeni Mwasha amesisitiza umuhimu wa Tanzania na Zambia kuimarisha ushirikiano katika kuondoa vikwazo vinavyoathiri biashara na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa baina ya nchi hizo.
Kwa upande wake, Dkt. Simon Ng’ona ameeleza umuhimu wa kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi ili kurahisisha biashara na usafirishaji wa bidhaa, hususan mazao ya kilimo, huku akieleza dhamira ya Zambia ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutatua changamoto hizo.
