Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUONGEZA KONGANI ZA VIWANDA KUIMARISHA UZALISHAJI


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga(Mb) amesema Serikali imepanga kuongeza maeneo maalum ya uwekezaji (kongani) nchini, hatua inayolenga kuchochea uzalishaji, kuongeza ajira na kuboresha mazingira ya kufanya biashara.

Akizungumza Novemba 24, 2025 jijini Dar es Salaam alipotembelea Tume ya Ushindani (FCC), Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema sekta ya viwanda imeendelea kukua na kuimarika, hususan katika uzalishaji wa malighafi unaochangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Waziri Kapinga amebainisha kuwa Serikali inaendelea kupanua wigo wa viwanda ili kukuza ajira, kuongeza mapato ya ndani na kupanua mauzo ya nje kupitia utekelezaji wa sera endelevu zinazolenga kukuza sekta hiyo.

Aidha, amesema kuimarishwa kwa viwanda kutachochea ongezeko la uzalishaji wa malighafi, hatua itakayoongeza mapato na kuendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa wawekezaji na wajasiriamali.

Waziri huyo ameongeza kuwa sekta ya viwanda inaratibu shughuli za sekta mbalimbali, na kwamba Serikali inaendelea kupunguza urasimu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau wa maendeleo.