Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUTEKELEZA MPANGO WA MIAKA 6 KUIMARISHA VIWANDA VYA NDANI NA KUPUNGUZA UTEGEMEZI WA BIDHAA ZA NJE


Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, imeanza mpango maalumu wa utekelezaji wa miaka 6 kuanzia 2025–2026 hadi 2030, kwa kuwekeza kwenye viwanda vya ndani, na kupitia mpango huo, kongani 52, yaani kongani 2 kwa kila mkoa, zitajengwa, na zitasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje.

Hadi kufikia mwezi Desemba 2025, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imefanikiwa kuanzisha kongani 36 katika mikoa 16 nchini. Kati ya hizo, kongani 6 zipo katika hatua ya ujenzi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), Bungeni jijini Dodoma Aprili 14, 2026 wakati akijibu swali namba 82. lililoulizwa na Mhe. Othman Maulid suleiman aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kuongeza Viwanda nchini ili kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

Akijibu maswali ya nyongeza Naibu Waziri Londo, amesema jukumu la kukuza, kuendeleza na kuhamasisha bidhaa za ndani ni jukumu la Watanzania wote, na kubainisha kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara, chini ya maelekezo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Taasisi ya TANTRADE, inaendelea kufanya mradi mkubwa wa kutangaza bidhaa zinazotengenezwa nchini, kupitia chapa ya “Made in Tanzania”.

Aidha, kupitia miradi mbalimbali ya uendelezaji wa viwanda, wanaendelea kutoa hamasa kwa Watanzania, na mwamko umeendelea kuwa mkubwa, hasa kwa viongozi wa Serikali, huku wakiendelea kuonekana wakitumia bidhaa za ndani, na kutoa rai kwa wabunge kuendeleza hamasa ya kutangaza bidhaa za Tanzania kwa kuzitumia na kuonyesha kwamba bidhaa hizo zina ubora na zinakidhi viwango.

Amesema kama ilivyo itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, wameendelea kutengeneza sheria na kanuni pamoja na kuboresha kanuni hizo, ikiwa lengo ni kulinda bidhaa za ndani na kuchochea uwekezaji na kuendeleza uzalishaji wa bidhaa za Tanzania, na kutolea mfano, wiki iliyopita Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, alivyoongoza zoezi la ukamataji wa bidhaa bandia zilizozalishwa chini ya viwango na kinyume cha taratibu.