Habari
SERIKALI KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUDHIBITI TAKA ZA PLASTIKI
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kunakuwa na uwiano kati ya udhibiti wa taka za plastiki, ulinzi wa mazingira na ukuaji wa sekta ya viwanda ili uchumi wa nchi uendelee kuimarika.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb) wakati wa mkutano wa wadau wa udhibiti wa taka za plastiki Agosti 04, 2026 jijini Dar es Salaam .
Kapinga amesema suala la taka za plastiki lina pande mbili muhimu kwani kwa upande mmoja linahusu uhifadhi wa mazingira na kwa upande mwingine linagusa shughuli za uzalishaji wa viwanda vinavyochangia ajira, mapato ya Serikali na maendeleo ya uchumi.
Aidha, kuna wazalishaji wa plastiki zinazotumika kama vibebeo na vifungashio vya matumizi ya kila siku pamoja na viwanda vikubwa vinavyotumia vifungashio vya plastiki katika bidhaa zao, hivyo ni muhimu kujenga mazingira yatakayowezesha sekta hizo kuendelea kufanya biashara huku zikizingatia sheria na kulinda mazingira.
Kapinga ameongeza kuwa Serikali inalenga kujenga mazingira yanayowiana kwa pande zote, ambapo wawekezaji watimize wajibu wao wa kulinda mazingira na mamlaka za udhibiti zitekeleze wajibu wake kwa njia wezeshi ili wadau wote waweze kufanya kazi kwa ushirikiano.
Hata hivyo Kapinga amevipongeza viwanda vinavyozingatia Sheria na taratibu za mazingira, akisema hatua hiyo imeviwezesha kudumu kwenye biashara kwa muda mrefu, amesema Serikali itaendelea kuviunga mkono na kuvipatia mazingira bora yatakayovichochea kukua zaidi na kuongeza mchango wake katika Uchumi wa Taifa.
Vilevile amesema Viwanda vinavyokiuka Sheria vinapaswa kutumia vikao vya wadau kama fursa ya kujikumbusha misingi ya sheria na kuelekezwa namna ya kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira ili viendelee kufanya biashara kwa ufanisi na kuongeza tija.
