Habari
SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI YA UWEKEZAJI NCHINI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, amesema Serikali kupitia wizara hiyo itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, kuwasimamia wawekezaji sambamba na kutatua changamoto zao ili viwanda hivyo viweze kuchangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Dkt. Hashil ameyasema hayo Novemba 15, 2025 Kigamboni, jijini Dar es Salaam, mara baada ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha dawa mbalimbali za mifugo cha Farm Base ambacho kimetajwa kuwa cha kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki.
Mapema, akizungumzia umuhimu wa kiwanda hicho kitakavyosaidia kuongeza ajira kwa vijana, Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Farm Base, Bw. Suleimani Msellem, amesema kiwanda hicho ambacho kinatarajiwa kufunguliwa mwezi Januari mwaka 2026 kitasaidia kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja.
Katika hatua nyingine, mkurugenzi huyo akizungumzia umuhimu wa vijana kujifunza teknolojia kupitia mitambo, amesema vijana wenye ujuzi wa mitambo hiyo bado ni wachache hapa nchini.
