Habari
Halmashauri zote nchini kutenga maeneo ya uwekezaji wa Viwanda ikiwa ni Mpango mahsusi wa Wizara wa kuhakikisha kila Mkoa na Halmashauri kunakuwa na Viwanda mbalimbali.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo (Mb) ameagiza Halmashauri zote nchini kutenga maeneo ya uwekezaji wa Viwanda ikiwa ni Mpango mahsusi wa Wizara wa kuhakikisha kila Mkoa na Halmashauri kunakuwa na Viwanda mbalimbali.
Ameyasema hayo Desemba 03,2024 ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika kiwanda cha Everwell Cable kinachotengeneza vifaa vya umeme ikiwemo Nyaya na Nguzo za zege kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani.
Dkt. Jafo amesema Wizara ya Viwanda na Biashara imeamua kujikita na ajenda hiyo ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuweka mazingira wezeshi na rafiki ili kuvutia wawekezaji wote wanaofika nchini,kujenga uchumi pamoja na kuhakikisha Serikali inapunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana kwenye kila Mkoa na Halmashauri zote na Taifa kwa ujumla.
Aidha Waziri Jafo amepongeza uwekezaji wa Kiwanda hicho ambao unazalisha nyaya za kilomita 500 kwa siku ambapo amesema uwekezaji huo utasaidia katika adhma ya Serikali ya kupeleka umeme vijijini.
Vilevile Waziri Jafo ametoa rai kwa vijana waliopata na watakaopata nafasi za ajira katika viwanda hivyo kuhakikisha wanakuwa waaminifu na wachapakazi kwa maendeleo yao binafsi na Taifa.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa kiwanda hicho Bw.Chang amesema lengo la kiwanda hicho ni kuhakikisha kinatengeneza vifaa vya umeme kulingana na mahitaji yaliyopo.