Habari
MAENDELEO YA VIWANDA MSINGI WA MAGEUZI YA KIUCHUMI- NAIBU WAZIRI LONDO
📌 Afungua Kongamano la Maendeo ya Viwanda nchini na Uzinduzi wa Programu ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Viwanda (PCP).
📌 Kongamano fursa ya kutafakari tulikotoka, tulipo na hatua tunazopaswa kuchukua ili kuharakisha maendeleo ya Viwanda nchini.
📌70% ya Uchumi wa Tanzania itategemea sekta binafsi - Dira 2050.
DODOMA
Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), amesema viwanda vya Tanzania vina nafasi kubwa katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, misitu, madini na rasilimali za bahari, kuzalisha ajira, kuongeza kipato cha wananchi, kupanua wigo wa mapato ya Serikali, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuongeza mauzo katika masoko ya kimataifa.
Mhe. Londo ameyasema hayo Novemba 3, 2026, jijini Dodoma, wakati akifungua Kongamano la Maendeleo ya Viwanda nchini na Uzinduzi wa Programu ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Viwanda, ikiwa ni kuelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 pamoja na Sera ya Maendeleo ya jasiriamali ndogo na za Kati ya mwaka 2003, Toleo la mwaka 2025, zitakazozinduliwa Novemba 4, 2026.
Ameongeza kuwa, tunapozungumzia maendeleo ya viwanda, hatuzungumzii kuongeza idadi ya viwanda pekee bali tunazungumzia mageuzi ya uchumi yanayoleta tija kwenye uzalishaji, ajira na ustawi wa wananchi.
Amesema Katika kuimarisha maendeleo ya viwanda nchini, Serikali imeandaa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 pamoja na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Mwaka 2003 (Toleo la 2025) zenye lengo la kuweka mwelekeo wa kuimarisha uzalishaji wa viwandani, kuongeza thamani ya malighafi za ndani, matumizi ya teknolojia na ubunifu, pamoja na kuboresha mazingira ya biashara, upatikanaji wa mitaji na masoko kwa wajasiriamali wadogo na wa kati. Hatua hii ni muhimu katika kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda na ujasiriamali katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha Mhe Londo ameongeza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kufanikisha miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga, pamoja na mradi wa Magadi Soda wa Engaruka. Miradi hii ina umuhimu mkubwa katika kuweka msingi wa kuanzisha viwanda vingine vinavyotegemea bidhaa zake, ikiwemo viwanda vya chuma na bidhaa zake, mashine na vifaa vya kilimo, vifaa vya ujenzi, bidhaa za kemikali, vioo na bidhaa nyingine zinazotumia magadi soda.
Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Balozi Waziri Rajabu Salum amesema kuwa kupitia kongamano hilo wanatarajia kupata maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu hatua za kuondoa vikwazo vya uwekezaji na uzalishaji, kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani na kubainisha miradi ya kipaumbele inayoweza kutekelezwa kupitia ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na washiriki wa maendeleo.
