Habari
VIWANDA NA BIASHARA YAOMBA BILIONI 137.8 KUIMARISHA UCHUMI WA VIWANDA
Wizara ya Viwanda na Biashara imeomba Bunge kuidhinisha jumla ya Sh bilioni 137.8 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kutekeleza mipango ya kuendeleza sekta ya viwanda na biashara nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo Mei 22, 2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 104.1 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida ya serikali.
Amesema kati ya fedha hizo za matumizi ya kawaida, Sh bilioni 78 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi wa wizara, huku Sh bilioni 26 zikitengwa kwa matumizi mengine ya uendeshaji wa shughuli za kila siku.
Kapinga amesema Sh bilioni 33.6 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo yote ikiwa ni fedha za ndani ya Serikali, hatua inayoonesha dhamira ya kuongeza uwekezaji katika sekta ya viwanda na biashara.
Amesema bajeti hiyo inalenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza uzalishaji wa viwanda vya ndani, kukuza biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.
