Habari
MFUKO WA VIWANDA, MIUNDOMBINU WEZESHI KUCHOCHEA MAENDELEO YA VIWANDA NA UJASIRIAMALI NCHINI
📌 Serikali inatarajia kuanzisha Mfuko wa Viwanda utakaosaidia wajasiriamali kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao.
📌 Sera mpya zinalenga kuboresha miundombinu wezeshi, upatikanaji wa mitaji na matumizi ya teknolojia.
📌 Sera zimezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na maoni ya wadau wa sekta zote.
Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (DSME), Eng. Simion Irege, amesema Serikali imehusisha wadau wa sekta za umma na binafsi katika mapitio ya Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Ndogo na wa Kati ya Mwaka 2003 (Toleo la Mwaka 2025), zinazotarajiwa kuzinduliwa Novemba 4, 2026.
Akizungumza Oktoba 27,2026 katika mahojiano na Crown FM kuelekea uzinduzi wa sera hizo, Mhandisi Irege amesema ushirikishwaji huo umelenga kuhakikisha sera zinazingatia mahitaji ya wadau na kuweka mazingira bora ya kukuza viwanda na ujasiriamali nchini.
Amesema sera hizo zimeweka mkazo katika kuboresha miundombinu ya maeneo ya biashara, kurahisisha upatikanaji wa mitaji na kuimarisha matumizi ya teknolojia mijini na vijijini kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) pamoja na taasisi nyingine za Wizara ya Viwanda na Biashara.
Kwa upande wake, Dkt. Yuda Benjamini, Mkurugenzi msaidizi Utafiti wa Viwanda, amesema Serikali inatarajia kuanzisha Mfuko wa Viwanda utakaosaidia wajasiriamali wadogo na wakubwa kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao, sambamba na kuboresha miundombinu wezeshi kwa ajili ya uzalishaji na biashara nchini.
Dkt. Yuda amesema maandalizi ya uzinduzi wa sera yamezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuoanisha ukuaji wa sekta ya viwanda na ujasiriamali na malengo ya maendeleo ya taifa.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano, utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda unatarajiwa kuchochea miradi ya kimkakati, ikiwemo Mchuchuma na Liganga kwa ajili ya uzalishaji wa chuma nchini, pamoja na mradi wa Soda Ash mkoani Arusha utakaowezesha upatikanaji wa kemikali zinazotumika katika viwanda mbalimbali.
Dkt. Yuda ameongeza kuwa sera hiyo inalenga kuboresha mazingira ya biashara na uzalishaji kupitia upatikanaji wa maeneo rasmi ya biashara, majengo, umeme na huduma za kuhifadhi na kuchakata malighafi. Pia, Serikali inalenga kukuza masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuongeza matumizi ya bidhaa za ndani na kusaidia viwanda vya Kitanzania kupanua uzalishaji.
Sera hizo zinatarajiwa kuweka mwelekeo wa kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza uzalishaji wa ndani na kuwawezesha wajasiriamali kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya viwanda na uchumi wa taifa.
