Habari
WAZIRI KAPINGA AITAKA SIDO KUONGEZA THAMANI YA MALIGHAFI, KUIMARISHA BIASHARA ZA WAZAWA
📌Afungua rasmi maonesho ya SIDO kwa mwaka 2026 wilayani Kahama;
📌Asisitiza unuhimu wa kuchakata malighafi kuongeza thamani badala ya kuuza bidhaa ghafi;
📌Serikali ya awamu ya sita kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya mikopo kwa wajasiriamali;
Kahama, Shinyanga
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amelitaka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kuongeza juhudi katika kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kupata teknolojia na mashine za gharama nafuu zitakazowawezesha kuongeza thamani ya malighafi, kukuza biashara na kutengeneza ajira nchini.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga ,wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya SIDO Kitaifa 2026 ambapo amesema,Tanzania ina utajiri wa rasilimali zinazotokana na kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na nyinginezo ambazo zinaweza kutumika kama msingi wa kuendeleza viwanda na biashara zenye tija na kusisitiza umuhimu wa kuchakata malighafi nchini ili kuongeza thamani badala ya kuuza bidhaa ghafi.
Kapinga ameitaka SIDO kuendeleza teknolojia rahisi zitakazowawezesha wananchi kuongeza thamani ya mazao kama kahawa na korosho, huku akisisitiza umuhimu wa SIDO kushirikiana na taasisi nyingine pamoja na sekta binafsi katika kubuni na kuboresha mashine zinazoweza kumudu kununuliwa na wajasiriamali wadogo.
Kuhusu upatikanaji wa mitaji, Kapinga amesema,Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuweka mazingira wezeshi kupitia mifuko na programu mbalimbali ili kuwawezesha mitaji hiyo ambapo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 14.572 ilitolewa kupitia SIDO, na asilimia 52 ya wanufaika walikuwa wanawake, huku ajira 13,482 zikihusishwa na jitihada hizo.
Amesema Serikali inalenga kuhakikisha huduma za mitaji na teknolojia zinaendelea kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi, hususani wale wenye uwezo wa kukuza uzalishaji na biashara zao lakini wanaokabiliwa na changamoto za kupata fedha za mitaji wanaendelea kuwawezesha ili kuongeza ushindani katika masoko ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Amesema serikali inataka kuona idadi ya wajasiriamali ikiongezeka na kujenga wajasiriamali wenye uwezo wa kuzalisha kwa tija, kujiajiri, kuajiri na kushindana sokoni na kukuza biashara kutoka hatua moja kwenda nyingine kupitia SIDO na ndiyo dhamira iliyopo
