Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

MAKAMPUNI WEKENI UWAJIBIKAJI KWA JAMII KATIKA MIKAKATI YA BIASHARA – LONDO


📌 Mafanikio ya kampuni yapimwe pia kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi, si faida pekee.

📌 Biashara endelevu zijenge uhusiano wa kudumu na jamii ili kuhakikisha uwepo wa soko la uhakika kwa vizazi vijavyo.

📌 Serikali na sekta binafsi zashauriwa kushirikiana kukuza viwanda, uwekezaji na uchumi jumuishi.

Dar es salaam

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Dennis Lazaro Londo (Mb), amezitaka kampuni na taasisi nchini kuweka uwajibikaji kwa jamii katika mipango na mikakati yao ya kibiashara ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaambatana na maboresho ya maisha ya Watanzania na maendeleo endelevu ya Taifa.

Mhe Londo ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, katika hafla ya Tuzo za Uwajibikaji kwa Jamii kwa Makampuni, Ukanda wa Afrika Mashariki, Awamu ya Tanzania 2026, ambapo amesema mafanikio ya kampuni hayapaswi kupimwa kwa faida inayopata pekee, bali pia kwa mchango wake katika jamii. 

“Katika biashara endelevu hatuwezi kupima mafanikio ya kampuni au taasisi kwa biashara inayofanya au kwa faida inayopata; biashara ni zaidi ya takwimu “ Alisema Mhe. Londo

Amesema uwajibikaji kwa jamii (CSR) ni nyenzo muhimu inayoiwezesha sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya nchi kwa kuongeza ajira, kuendeleza ujuzi, kuboresha huduma za elimu na afya, kuhifadhi mazingira na kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi. 

Aidha Mhe Londo aliongeza kuwa  wajibu wa mzalishaji si kutoa bidhaa na huduma pekee, bali pia kuchangia ustawi wa jamii na kujenga mazingira rafiki kwa biashara za sasa na zijazo na kusisitiza kampuni zinapaswa kuangalia zaidi manufaa ya muda mrefu kwa kujenga uhusiano endelevu na jamii zinazozunguka shughuli zao.

Ameeleza kuwa jamii yenye ustawi ni sehemu muhimu ya maendeleo ya biashara ma kuhimiza makampuni kuwekeza katika vipaji na ujuzi wa Watanzania na kutoa fursa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia maboresho ya miundombinu ya barabara, reli, bandari, mawasiliano na nishati, hatua zinazolenga kurahisisha usafirishaji, uzalishaji na shughuli za biashara na kusisitiza maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa na Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za umma, vyama vya wafanyakazi na wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Orange CSR Research Worldwide, Bi. Suzan Kanga amesema Orange CSR itaendelea kuunga mkono na kutambua taasisi mbalimbali na kuleta mabadiliko chanya katika jamii ili kubadilisha maisha ya wananchi.

Pia amezipongeza na kuziasa taasisi zilizopewa tuzo ziendelee kutumikia wananchi kwa manufaa ya maendeleo ya nchi nzima.

Katika hafla hiyo, Londo amewapongeza Orange CSR Research Worldwide kwa kuandaa tuzo hizo zinazolenga kutambua, kuthamini na kuhamasisha mchango wa kampuni na taasisi katika maendeleo ya jamii na amewapongeza washindi na wote waliotambuliwa, huku akiwahimiza kuendeleza juhudi zao, akisisitiza kuwa thamani ya uwajibikaji kwa jamii haipimwi kwa tuzo pekee, bali kwa mabadiliko halisi na endelevu katika maisha ya wananchi.