Habari
TAASISI ZINAZOHUSIKA NA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA ZAT AKIWA KUSHIRIKIANA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga amezitaka Taasisi na Wadau wakiwemo Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bodi za mazao, Waendesha Maghala pamoja na Taasisi za kifedha wanaofanya kazi na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala waendelee kushirikiana kwa karibu ili kuimarisha na kukuza Mfumo huo uendelee kuwa na tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Vile vile amesema Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umeendelea kuthibitisha kuwa ni nyenzo sahihi ya kuleta ahueni kwa wakulima, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kupitia biashara yenye uwazi na ushindani.
Kapinga amesema hayo Mei 18, 2026 wakati akifungua Mijadala na Uzinduzi wa Jarida kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 20 ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Amesema chini ya uongozi wa Rais wakati Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara, kuimarisha mifumo ya masoko na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini.
“Katika miaka 20 ya uwepo wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), tumethibitisha kuwa mfumo huu una manufaa makubwa kwa wakulima na wafanyabiashara. Wadau wengi sasa wanajadili namna ya kuuboresha zaidi badala ya kuhoji umuhimu wake,” amesema.
Aidha, ameahidi kuwa Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) pamoja na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji wa maghala na huduma zinazohusiana na mfumo huo.
