Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira yaipongeza BRELA kwa kuboresha utendaji kazi.


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof Kitila Mkumbo (Mb) Serikali itaendelea kuiwezesha BRELA kuboresha utoaji wa huduma zake kwa wafanyabiashara kwa kuwa ni chombo muhimu katika ukuaji wa Sekta ya Biashara nchini.

Waziri Mkumbo ameyasema hayo wakati wa semina iliyolenga kuwaelimisha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Viwanda Biashara na Mazingira kuhusu utekelezaji wa majukumu ya BRELA na mafanikio yake iliyofanyika tarehe 9 Juni 2021 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Nayo, Kamati hiyo imeipongeza BRELA kwa kuboresha utendaji kazi  na kuitaka iendelee kuongeza ubunifu katika kuboresha huduma na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hizo hadi vijijini.

Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo  walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali  yanayolenga kuboresha huduma na bidhaa zinazotolewa na BRELA ikiwemo Uhuishaji wa taarifa, uhusiano wa biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, Umiliki Manufaa na Sera ya Taifa ya Umiliki Binafsi

Akiwaelimisha Wajumbe wa Kamati hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bwana Godfrey Nyaisa alisema BRELA inaendelea kuboresha utoaji wa huduma zake kwa njia ya mtandao kwa kutumia mifumo mbalimbali ya Sajili kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Bwana Nyaisa pia alisema BRELA inaendelea kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mtaa na SIDO katika utoaji wa huduma, na imeingia makubaliano mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa katika nyanja za umiliki wa ubunifu.

Alisema jukumu la msingi la BRELA ni kusimamia ufanyikaji wa Biashara nchini kwa kuzingatia sheria na kanuni za biashara zilizopo.

Afisa huyo alisema ili kuhakikisha kuwa mazingira ya uwekezaji, uanzishaji na urasimishaji biashara nchini yanakuwa wezeshi, BRELA imeandaa Mpango Mkakati wa saba unaoanza kutekelezwa mwaka 2021/22 na unalenga kuboresha utoaji wa  huduma za sajili na leseni ili kuwa na ukuaji endelevu wa viwanda na maendeleo ya uchumi.

Alisema mpango huo umelenga kufanya maboresho ya sheria zinazosimamiwa  na BRELA ili kuendana na mahitaji ya kibiashara ya sasa na mipango ya kitaifa.

Akitaja mambo yaliyotekelezwa hadi sasa katika mpango mkakati wa sita, Bwana Nyaisa alisema kuweka mifumo ya Kielektroniki ya Utoaji wa Huduma za Sajili (ORS) na Utoaji wa Leseni za Biashara (NBP).

Pia alitaja utengenezaji na uboreshaji wa mifumo ya utendaji  kazi kama Mfumo wa ki-elektoniki wa Majalada – “e-Office”, Matumizi ya Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE), na Mfumo wa ki-elekroniki wa mahudhurio (e- Attendance   System).

Bwana Nyaisa alisema pia uandaaji wa nyaraka mbalimbali za Kiutendaji na  Kiutawala kama Mpango Mkakati – Strategic Plan   2021/22– 2025/26, Mkakati wa Mawasiliano na Huduma kwa   Mteja   (Communication and Customer Service Strategy), Kanuni za Utumishi, Fedha, na maendeleo ya Watumishi.