Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WIZARA, MABALOZI WATEULE WA TANZANIA NJE YA NCHI KUSHIRIKIANA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA


Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kibiashara na Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi ili kuhakikisha vikwazo vya kibiashara kimataifa vinaondolewa kwa wakati na ufanisi mkubwa na kuchochea ukuaji wa Viwanda nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Waziri Salum, Aprili 17, 2026, jijini Dar es Salaam alipofanya mkutano na Mabalozi Wateule watakaoiwakilisha Tanzania katika mataifa ya Jamhuri ya Korea, Comoro, Sweden, Saudi Arabia, Zambia, Oman, na Umoja wa Mataifa.

Aidha, Balozi Salum amesisitiza kuwa uhusiano imara wa kibiashara unategemea sana mawasiliano ya haraka ya Taarifa na takwimu sahihi.

Vilevile amewashauri Mabalozi hao kutangaza fursa za viwanda na biashara zilizopo nchini ili Tanzania inufaike kiuchumi kupitia wawakilishi wake waliopo nje ya nchi.

Kwa upande wao, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Aristides Mbwasi, na Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Bw. Needpeace Wambuya, wameeleza kuwa ushirikiano huu ni msingi wa matokeo yanayoonekana, huku changamoto zikitafutiwa suluhu kupitia Kamati za Pamoja (JTC).

Nao Mabalozi wateule wameahidi ushirikiano wa dhati na kutoa ushauri wa kimkakati ili kuhakikisha biashara za Tanzania zinastawi katika masoko ya nje ya nchi.