Habari
ZIARA YA WAZIRI KAPINGA NCHINI CHINA YAZAA MATUNDA, YAIVUTIA KAMPUNI KUBWA KUWEKEZA TANZANIA.
Kufuatia ziara rasmi nchini China iliyofanywa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), Machi 2026, ambapo Tanzania ilitangazwa kama kivutio cha uwekezaji wa viwanda, kampuni ya HONGDESHENG (Fujian) Investment Group Co. Ltd imeonesha nia ya kuwekeza nchini.
Kufuatia ziara hiyo, Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Bw. Lin Xiang Rong, pamoja na watendaji wake, wamewasili nchini Aprili 16, 2026 na wamekutana na Waziri wa Viwanda na Biashara kujadili mradi wa uwekezaji wa kiwanda cha chuma, sambamba na kutoa shukrani kwa ziara yake nchini China.
Mradi huo unatarajiwa kuwa na uwekezaji wa dola za Marekani milioni 70 hadi 90, ukiwa na uwezo wa kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka. Bidhaa zitakazozalishwa ni nondo na bidhaa mbalimbali za chuma.
Ujenzi wa kiwanda unatarajiwa kuanza Juni 2026 na kukamilika ndani ya miezi 18, huku uzalishaji ukitarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka 2027.
Mradi huu unatarajiwa kutoa ajira zipatazo 400 za moja kwa moja, pamoja na ajira nyingine zisizo za moja kwa moja. Sambamba na kuchochea maendeleo ya sekta za ujenzi, madini na viwanda.
Kwa ujumla, mradi huu unachangia juhudi za Tanzania za kuimarisha sekta ya viwanda, kuongeza uzalishaji wa ndani na kukuza uchumi wa Taifa.
