Habari
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo yaiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha Tanzania inaonekana katika maandalizi ya Kuridhia Itifaki ya Biashara Kusini mwa Afrika

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha kuwa manufaa Tanzania yanaonekana katika maandalizi ya Kuridhia Itifaki ya Biashara na Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
Hayo yamesemwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Medard Kalemani,(Mb.) Agosti 15, 2023 wakati Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwasilisha Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Biashara na Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kutoa maoni mbalimbali kuhusu utayari wa Tanzania katika kuridhia Itifaki hiyo ya Biashara na huduma ili kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na itifaki hiyo.
Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe(Mb.) akijumuisha maoni na mapendekezo hayo ameihakikishia Kamati hiyo kuwa maelekezo na mapendekezo yote yaliyotolewa yatazingatiwa katika utekelezaji wa Itifaki hiyo ili kuchochea uchumi na biashara miongoni mwa Nchi wanachama kwa kuondoleana vikwazo na kulegezeana masharti na taratibu mbalimbali za utoaji huduma.
Aidha, alibainisha kuwa Tanzania ikiridhia Itifaki hiyo itafaidika kwa kuongeza uzalishaji kwa wakulima, ajira na thamani ya mazao ya kilimo, soko kubwa la bidhaa lenye watu takribani milioni 360, kuongezeka kwa tija na ubora wa bidhaa na huduma za Tanzania kutokana na ushindani, upatikanaji wa bidhaa na huduma mbalimbali nchini pamoja na uhawilishajinwabteknolojia kutoka nje ya nchi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara aliieleza Kamati hiyo kuwa Itifaki hiyo ilianza kutumika Januari 13, 2022 baada ya nchi 11 kati ya 16 Wanachama wa SADC kuridhia na kuipa nguvu ya kisheria kuanza kutekerezwa.
Aidha Alieleza baada ya Itifaki hiyo kusainiwa na Nchi Wanachama Agosti, 2012 zilianza majadiliqno kwa awamu ya kwanza ya Biashara ya Huduma katika maeneo ya Mawasiliano, Fedha, Utalii, Uchukuzi, Nishati,na Ujenzi wakati Awamu ya Pili ni Usambazaji, Elimu, Mazingira Afya ya Jamii Burudani na Utamaduni na Michezo