Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda,Biashara,Kilimo na Mifugo yazipongeza TBS na WMA


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda,Biashara,Kilimo na Mifugo imezipongeza Shirika la Viwango Tanzania,Tume ya Ushindani na Wakala wa Vipimo Tanzania kwa kutekeleza majukumu yao katika Bandari ya Dar es Salaam.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Mariam Ditopile Mzuzuri kwaniaba ya kamati wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kuona majukumu ya Taasisi hizo katika Bandari ya Dar es Salaam Oktoba 07,2024.

Mhe.Ditopile amesema utendaji kazi wa Taasisi hizo chini ya Wakuu wa Taasisi ni kazi nzuri inayofanywa na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha usalama wa bidhaa zinazotumiwa na Watanzania, Usawa wa biashara pamoja na kuhakikisha uhamasishaji wa uwekezaji wa Viwanda na kupelekea bidhaa kupata soko.

Aidha Mhe.Ditopile amezitaka Taasisi za Wizara ya Viwanda na Biashara na Taasis za Wizara nyingine ndani ya Serikali pamoja na Mwekezaji kukaa pamoja na kufanya mifumo isomane ili kufikia dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan ya kuongeza watumiaji wa bandari na kuchochea uchumi wa Nchi na kuongeza ajira.

Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe.Exaud Kigahe(Mb) ameishukuru kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo na ushauri uliotolewa na kamati hiyo ili kuendelea kurahisisha utendaji wa taasisi hizo.

Vile vile Mhe.Kigahe amesema lengo la Wizara kupitia Taasisi zake hizo ni pamoja na kufanya kazi kwa haraka ili kuhakikisha kunakuwa na bidhaa zenye ubora zinazotoka ndani na nje ya nchi pamoja na kuondoa bidhaa bandia ili kupata watumiaji wengi wa bandari hiyo ili kuongeza uchumi wa nchi.