Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TUZO ZA WAFANYABIASHARA KARIAKOO KUKUZA BIASHARA ZINAZOAMINIKA


Serikali imewahakikishia Wafanyabiashara kuwa Serikali itaendelea kusikiliza na kutafuta changamoto zao na kuhakikisha wanapata mazingira yenye utulivu, uwazi na usalama wa mitaji yao.

Vilevile itaendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kuhakikisha wafanyabiashara wa Kariakoo wanakuwa na ushindani wa kikanda na kimataifa huku ikiitaja Kariakoo kuwa moyo wa biashara wa Tanzania na injini muhimu ya uchumi wa taifa.

Hayo yameelezwa Mei 17, 2026 katika hafla ya Utoaji wa Tuzo za Biashara Kariakoo jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Mbwasi, aliyemwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Mhe Judith Kapinga

Aidha Mbwasi amesisitiza kuwa Kariakoo si eneo la kawaida katika historia ya biashara nchini bali ni alama ya uchapakazi, uthubutu na mafanikio ya Watanzania wengi.

Amesema Kariakoo imekuwa sehemu iliyojenga maisha ya maelfu ya wananchi, huku vijana wengi wakianza biashara kwa mitaji midogo na baadaye kuwa waajiri wakubwa.

“Kila siku maelfu ya watu wanaingia Kariakoo kufanya biashara, kununua bidhaa, kuwekeza na kusafirisha bidhaa kwenda ndani na nje ya nchi ikiwemo DRC, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi, Uganda na Comoro,” amesema.

Akizungumzia ujenzi wa Soko Kuu la Kariakoo baada ya janga la moto, amesema Serikali ilihakikisha soko hilo linajengwa upya kwa kiwango kikubwa zaidi ambapo mradi huo uligharimu takribani shilingi bilioni 28 na kuwa na zaidi ya maduka 2,000.

Amesema Serikali inaamini sekta binafsi ni mshirika mkuu wa maendeleo ya uchumi, ndiyo sababu imeendelea kuboresha mazingira ya biashara, kurahisisha uwekezaji, kupanua miundombinu ya masoko na kuimarisha huduma za kidigitali.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kariakoo Business Awards, Zakayo Shushu, amesema tuzo hizo zimeanzishwa kwa lengo la kutambua ubunifu, uwekezaji na juhudi za wafanyabiashara wanaofanya biashara kwa uaminifu na weledi mkubwa.

Amesema tuzo hizo zinalenga kukuza biashara zinazoaminika pamoja na kuchochea ushindani wa kitaalamu ili wafanyabiashara wa Kariakoo waweze kushindana katika soko la ndani na la kimataifa.