Habari
LONDO: KAZI YA SERIKALI KUMSAIDIA MTANZANIA KWENYE MABADILIKO YA UCHUMI
Serikali imesema itaendelea kumsaidia mtanzania kushiriki kwenye mabadiliko ya kiuchumi kwa kusimamia bidhaa za ndani kupata soko zaidi kuliko zinazotoka nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo (Mb) wakati wa ziara yake ya siku moja katika Kiwanda cha kuzalisha chanjo za mifugo cha Hester na Kiwanda cha kuunganisha magari cha GF Vehicle Assembler vilivyopo Kibaha Mkoani Pwani.
Londo amesema wawekezaji wa ndani wanatakiwa kuanza kuzalisha bidhaa nyingi zaidi ili kukidhi mahitaji ya ndani na ya Viwanda vingine na Serikali inaendelea na utaratibu wake wa kudhibiti uingizwaji bidhaa ambazo hazizalishwi ndani ya nchi ili kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Vilevile ameongeza kuwa Serikali inajipanga kwa kushirikiana na wadau wa ndani waanze kuzalisha bidhaa ambazo zinatumiwa na viwanda vingine ili kupunguza kuingiza kutoka nje.
Aidha Amepongeza uwekezaji wa viwanda hivyo kwa namna inavyoinua uchumi wa Taifa na kutoa ujuzi na ajira kwa vijana nchini.
Kwa upande wa Meneja Mkuu wa Kiwanda cha GF Vehicle Assembler Ndg. Ezra Mereng amesema zaidi ya vijana 200 wananufaika na kiwanda hicho ambapo asilimia 99 ni wazawa
Naye Mkurugenzi wa Kiwanda cha kuzalisha chanjo za mifugo cha Hester Bi. Christine Sokoine amesema kwamba tayari aina 12 za chanjo zimeshasajiliwa na zinauzwa ndani na nje ya nchi ikiwemo Kenya, Israel, Namibia,Ghana,Burundi na Zambia.
