Habari
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kukamilisha zoezi la mchakato wa kupata chapa ya ‘ MADE IN TANZANIA
Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Dkt. Selemani Jafo(Mb) ameiagiza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kukamilisha zoezi la mchakato wa kupata chapa ya ‘ MADE IN TANZANIA’ ndani ya miezi mitatu ili iweze kuzinduliwa rasmi katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (sabasaba).
Amebainisha hayo wakati wa hafla ya kutangaza bunifu zilizoshinda nembo ya ‘MADE IN TANZANIA ‘ uliofanyika katika ukumbi wa Mwl.Julius Nyerere International Convention center ( JNICC) Februari 11,2025.
Amesema lengo la kufanya haraka kupata nembo hiyo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na nembo yake katika bidhaa kwaajili ya kutangaza bidhaa zote za nchi katika masoko mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, kuweka ushindani na kusaidia katika takwimu.
Aidha Waziri Jafo amewaagiza majaji wafanye ushindanishi wa haraka kati ya chapa ambazo zimeingia tatu bora ili kupata ambayo inafaa kutumika na kuipa nchi thamani ya kuwa na bidhaa zitakazo tambulika kimataifa.
Vilevile Dkt. Jafo ametoa agizo kwa Tantrade kuhakikisha mshindi wa chapa hiyo anapewa motisha ya kipekee ili kuwa chachu kwa wengine yanapotokea mashindano kama hayo.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Ndg.Sempeho Manongi amesema, lengo la bunifu hiyo ni kutambulisha bidhaa za ndani na nje ya nchi na pia Dunia ktambua Tanzania inauwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa zenye ubora.
Naye Mkurugenzi wa Tantrade Bi. Latifa khamis amesema mchakato huo wa kuweza kutafuta nembo ambayo itakuwa ni kiwakilishi cha Tanzania katika bidhaa umekuwa wa muda mrefu na imeshirikisha sekta binafsi, na hivyo ni muhimu kuwa na nembo Kwa lengo la bidhaa za Tanzania kupata haki ya ubora Duniani.