Habari
MARKUP II KUKUZA MNYORORO WA THAMANI NA AJIRA
Mradi wa Uongezaji Thamani Katika Mazao ya Kimkakati kwa Ajili ya Masoko ya Ndani na Nje ya Nchi (MARKUP II) unatarajiwa kuwezesha ukuaji mkubwa wa mnyororo wa thamani katika uzalishaji na kuongeza ajira, hususan katika sekta ya viwanda vidogo nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ya Zanzibar Dkt. Said Seif Mzee, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Hashil Abdalla, Oktoba 15 Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Taifa wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa MARKUP II.
Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo katika awamu iliyopita kwa kipindi cha miaka minne (2023-2027), kwa ushirikiano na Shirika la Biashara la Kimataifa (ITC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Dkt. Seif amesisitiza kuwa mradi wa MARKUP II umetokana na mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika awamu ya kwanza (MARKUP I). Aidha, ameongeza kuwa mradi huu unajumuisha fursa za masoko na uwezo wa kuyafikia masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi.
Jambo hili litafaidisha viwanda vidogo ambavyo hutoa ajira na mchango mkubwa kiuchumi katika nchi za EAC. Maeneo yaliyolengwa na mradi katika awamu hii ni uongezaji thamani katika mazao ya Kahawa, ngozi, parachichi, viungo vya chakula na kinywaji pamoja na suala la vifungashio.
Kwa upande wa Tanzania, MARKUP II inalenga hasa kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya Kahawa, bidhaa za ngozi na vifungashio. Mradi huu unahusisha nchi za EAC ambazo ni Tanzania, Burundi, Kenya, Uganda, Rwanda na Sudan Kusini, kama alivyoeleza Mratibu wa mradi kutoka ITC, Bw. Safari Fungo.
Mkutano huo pia umepokea taarifa fupi juu ya maandalizi ya Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Kikanda utakaofanyika Bujumbura, Burundi, kuanzia Novemba 3 hadi 5, 2025. Maazimio ya mkutano huu wa kitaifa yatakuwa msingi mkuu wa majadiliano na maazimio katika mkutano huo wa kikanda huko Burundi.
