Habari
WAZIRI KAPINGA ATAKA KUONGEZA KASI YA PROGRAMU ZA VIWANDA KUFIKIA AJIRA MILIONI 8
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amezitaka taasisi zote kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa kipindi cha miaka mitano kimeanza na mategemeo ya kuzalisha ajira milioni nane. Amesema programu zilizopangwa zinapaswa kuharakishwa ili kufikia malengo hayo kwa wakati.
Akizungumza leo Novemba 26, 2025, katika ziara yake Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Waziri Kapinga amesema taasisi zinapaswa kushirikiana kwa ukaribu na Wizara ya Vijana, ambayo ndiyo mratibu wa programu hizo, na kuwa na wepesi na umakini katika kuhakikisha shughuli zinazohusu vijana zinaendeshwa kwa ushirikiano mpana na wenye tija.
Aidha, ameeleza kuwa uanzishaji wa mitaa ya viwanda katika kila wilaya unahitaji ushirikiano wa taasisi mbalimbali, ambapo TIRDO ina nafasi muhimu kutokana na uwezo wake wa kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kiteknolojia. Amesema viwanda vinahitaji mazingira sahihi na uelewa wa soko ili kuhakikisha uzalishaji wa ajira unaendana na mahitaji ya wakati.
Waziri Kapinga ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea kila siku, huu ni wakati kwa TIRDO kusaidia taasisi nyingine na programu mbalimbali ili kuhakikisha mipango inatekelezwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na mwelekeo wa ukuaji wa viwanda nchini.
