Habari
WAZIRI KAPINGA AIAGIZA BRELA KUONGEZA KASI NA UBUNIFU KATIKA HUDUMA
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga amesisitiza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kufanya kazi kwa kasi na ubunifu katika utoaji wa huduma kwa Wafanyabiashara ili kufikia malengo yanayotarajiwa na Wafanyabishara.
Akizungumza na Menejimenti ya BRELA Novemba 27, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri Kapinga ameiagiza BRELA kuendelea kuelimisha jamii, kufanya ukaguzi wa biashara ili kuleta ufanisi na kuweka mazingira wezeshi kwa biashara.
Aidha, Waziri Kapinga ameipongeza BRELA kwa kuboresha mifumo ya kidijitali na uendeshaji wa shughuli zake kulikoongeza usajili wa biashara na leseni.
Waziri Kapinga pia ameipongeza BRELA katika kipindi cha miaka mitano BRELA imeongeza gawio lake kwa Serikali kwa kuchangia kiasi cha takribani shilingi bilioni 82.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa amesema wamepokea maelekezo na Wako tayari kuyatekeleza hususani katika kuboresha mifumo ambayo inaunganishwa na taasisi nyingine na kuwajengea uwezo watumishi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.
Aidha, Bw. Nyaisa amebainisha kuwa mpaka sasa mifumo ya BRELA inasomana na taasisi mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), NIDA na baadhi ya benki nchini jambo linaloongeza ufanisi na kuondoa ulazima wa kufuata huduma kwenye kila Ofisi.
