Habari
WAZIRI KAPINGA AIAGIZA SIDO KUTUMIA MIFUMO YA KIDIJITALI NA KUONGEZA UBUNIFU
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kuongeza ubunifu na kutumia mifumo ya kidijitali katika utekelezaji wa shughuli za shirika hilo.
Waziri Kapinga meyasema hayo Novemba 26, 2025 wakati alipotembelea shirika hilo na kuzungumza na Bodi pamoja na Menejimenti ya SIDO huku akiahidi kutoa ushirikiano ili kuwezesha viwanda vidogo na biashara ndogo kukua na kuongeza ajira kwa vijana.
Aidha, amefafanua kuwa mifumo hiyo ya kidijitali itasaidia kuwa na idadi sahihi ya viwanda vidogo na kuisadia Serikali kupanga mikakati ya maendeleo kwa ufanisi.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera amebainisha SIDO ni uti wa mgongo wa viwanda vidogo na mshirika muhimu wa Serikali katika uchumi wa viwanda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya SIDO, Prof. Mussa Nyamsingwa, amesema SIDO iko tayari kupokea maelekezo na kuyatekeleza kwa ufanisi ili kuhakikisha mpango wa kuinua sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo unafanikiwa na kuzalisha ajira kwa vijana.
