Habari
MSIPANDISHE BEI ZA BIDHAA KATIKA MSIMU WA SIKUKUU: PROF. MKUMBO
Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo ametoa rai kwa wafanyabiashara nchini kutopandisha bei za bidhaa katika msimu huu wa sikukuu za krismasi na Mwaka mpya.
Prof. Mkumbo ametoa rai hiyo wakati akizindua duka jipya la nguo la kampuni ya LC Waikiki lililopo Mlimani city Dar es salaam. Disemba 13, 2021.
“Wafanyabiashara duniani kote wakati wa sikukuu huwa wanashusha bei, tunatarajia na wafanyabiashara wa Tanzania wastaarabike badala ya kupandisha bei wakati wa sikukuu, ni muda mzuri wa kushusha bei ili kila mwananchi aweze kufurahia sikukuu” amesema Prof. Kitila Mkumbo
Wakati akizundua duka hilo, Prof. Mkumbo amesema ufunguzi wa duka hilo unaongeza biashara ambayo itachangia kulipa kodi ya Serikali kupitia mauzo vilevile kutoa ajira ambapo kwa sasa wameshaajiriwa Watanzania 50.
Aidha, Prof. Mkumbo ameeleza kuwa kampuni LC Waikiki mpaka sasa ina biashara 1,152 duniani kote hivyo uwekezaji huo nchini umetokana na juhudi za serikali kuweka mazingira mazuri kuwekeza na kufanyabiashara.