Habari
WANANCHI WA MTWARA WAI SHUKURU SERIKALI KWA UJENZI WA SHULE ZA KISASA NA WODI YA WAZAZI
Wananchi wa Mkoa wa Mtwara wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa shule za kisasa za Msingi na Sekondari pamoja na wodi ya wazazi, hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto za upatikanaji wa elimu na huduma za afya kwa wananchi wa mkoa huo.
Shukrani hizo zimetolewa Agosti 11, 2026 mbele ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu Mkoani Mtwara yenye lengo la kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Katika ziara hiyo, ametembelea majimbo ya Lulindi, Newala Mjini, Newala Vijijini na Tandahimba.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Shule mpya ya Msingi Chilimba iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Bi. Magreth George amesema kuwa mradi huo utawawezesha watoto kusoma katika mazingira salama na ya kuaminika, huku ukiondoa changamoto ya kuathiriwa na mvua wakati wa masomo.
Akiwahutubia wananchi waliojitokeza katika ziara hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesisitiza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuendelea kutenga fedha na kutekeleza miradi mingine ya kimkakati ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, Mhe. Kapinga amewataka wananchi kupima mafanikio ya Serikali kupitia matokeo halisi ya miradi ya maendeleo, badala ya kuyumbishwa na kauli za upotoshaji.
Pia amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuisemea vyema, akibainisha kuwa maendeleo makubwa yanayopatikana yametokana na ushirikiano imara kati ya wananchi na Serikali.
