Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt. Selemani Jafo (Mb) ametoa rai kwa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) kushirikiana kwa sauti moja yenye nguvu bila kujenga matabaka yoyote katika kutekeleza Mkataba huo ambao utaiwezesha Afrika kujitegemea na kuleta maendeleo ya Kiuchumi, Kisiasa na Kiutamaduni kwa Afrika na wananchi wake.
Vilevile, ametoa wito kwa Nchi hizo kuhakikisha zinatekeleza kwa vitendo makubaliano katika Mkataba huo ili kuweza kujitegemea ndani ya Afrika, kupunguza madhara ya misukosuko ya uchumi wa dunia na kuweka mikakati imara katika kuifikia ajenda 2063 ya Afrika tuitakayo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Waziri Jafo amayesema hayo Novemba 9, 2024 akiwa kama Mwenyekiti wa Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri wa AfCFTA wa wakati akihutubia hafla ya ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika Novemba 9, 2024, Addis Ababa, Ethiopia ambapo Tanzania ni Mwenyekiti wa Mikutano ya AfCFTA kwa mwaka 2024.
Aidha, Waziri jafo ameeleza jinsi Tanzania inavyochukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto za ufanyaji biashara chini ya AfCFTA kama ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, Mradi wa Bwawa la umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ujenzi wa viwanja vya ndege, miundombinu ya barabara, uboreshaji wa bandari za Dar es salaam, Tanga, na Mtwara, uimarishaji wa mifumo ya kidigitali na urekebishaji wa Sera ya Biashara mwaka 2003 kuwa na toleo la 2023.
Naye Rais wa Jamhuri ya Ethiopia Mhe. Taye Atske Selassie amesisitiza kuwa AfCFTA ni zaidi ya mkataba wa biashara bali ni chombo chenye nguvu kitakachosukuma ukuaji wa kiuchumi, kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika, kuongeza biashara na ajira, kupunguza umasikini, na kuharakisha utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika
Vilevile, Katibu Mkuu wa AfCFTA Mhe. Wamkele Mene amesisitiza Nchi Wanachama kuendelea kuboresha sera, kurahisisha ufanyaji biashara, kukuza ushirikiano imara kati ya sekta za umma na binafsi, kuendesha wa Mfumo wa Malipo na Makubaliano ya Kanda Huru ya Afrika (PAPSS), kuendeleza Mfuko wa Marekebisho wa AfCFTA na kuendeleza Jukwaa la Biashara Afrika.