Habari
PROF. MKUMBO AHITIMISHA MAADHIMISHO YA KITAIFA YA SIKU YA USHINDANI DUNIANI 2021.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo ameeleza kuwa madhumuni ya Serikali katika kusimamia uchumi wa soko si kukataza biashara bali kutaka ifanyike kwa kuzingatia sheria na misingi ya ushindani.
Prof. Mkumbo ameeleza hayo leo Disemba 06, 2021 wakati akihitimisha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya ushindani duniani chini ya kauli mbiu “Ushindani na Ujenzi wa Uchumi Jumuishi na Stahimilivu” yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere, Dar es salaam.
“Serikali ilianzisha Tume ya Ushindani ili kuhakikisha kunakuwa na ushindani wa halali miongoni mwa washindani (wazalishaji na wafanyabiashara) vilevile kuhakikisha mlaji analindwa” amesema Prof. Kitila Mkumbo
Prof. Mkumbo amesema kuwa kutokana na mahitaji ya Tume ya Ushindani kwa utekelezaji bora zaidi wa sheria huska, Wizara imekusudia kupeleka Bungeni muswaada wa marekebisho ya sheria ya ushindani ili kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wake na kutoa mwanya kwa washiriki wa uvunjaji wa sheria wa maswala ya ushindani kujisalimisha FCC.
Aidha, Prof. Mkumbo amesema kuwa maadhimisho ya kitaifa ya siku ya ushindani ulimwenguni ni suala la muhimu ambalo linapaswa kuendelea kufanyika na wigo wake kupanuliwa ili liweze kuwafikia wadau wengi Zaidi nchini.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani, William Erio ameeleza kuwa siku ya ushindani duniani hufanyika Disemba 05, kila mwaka ambapo mwaka huu imeadhimishwa kwa kufuata kauli mbiu ya ushindani kwa uchumi jumuishi na himilivu.