Habari
PROF. MKUMBO : CHUO CHA CBE KIJIKITE KUTOA ELIMU YA BIASHARA KWA WAJASIRIAMALI, KUTOA WAHITIMU WENYE UJUZI KULINGANA NA MAHITAJI YA SOKO NA KUANDAA MAFUNZO KWA MAAFISA BIASHARA.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) ameiagiza Bodi ya Uongozi wa Chuo cha Biashara (CBE) kusimamia Chuo katika utoaji wa huduma bora katika jamii kwa kutoa elimu ya biashara kwa wajasiriamali, kutoa wahitimu wenye ujuzi kulingana na uhitaji wa soko na kutoa mafunzo na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Maafisa biashara.
Prof. Mkumbo ameyasema hayo Julai 12, 2021 katika hafla fupi ya uzinduzi wa Bodi ya Uongozi wa Chuo cha Biashara (CBE) iliyofanyika katika Chuo hicho Dar es salaam na kuhudhuliwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Doto James, Mkuu wa Chuo cha CBE Prof. Emanuel Mjema na Uongozi wa Wanafunzi wa Chuo hicho.
Prof. Mkumbo aliitaka Bodi hiyo kuandaa mpango wa upimaji wa matokeo kwa kuzingatia maeneo matatu ya majukumu ya Bodi ambayo ni kutoa ushauri katika maeneo yenye tija kwa Taasisi ndani na nje ya vikao vya Bodi, kuwa mtunza nidhamu wa Mkuu wa Taasisi na Menejimenti ya Taasisi kwa niaba ya mmiliki wa Chuo ambayo ni Serikali na kutoa utatuzi pale Taasisi inapokuwa inakabiliwa na changamoto za kimenejimenti.
Aidha, Prof. Mkumbo aliiasa Bodi kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuzingatia uelewa mzuri wa maana, malengo, na majukumu ya Taasisi, sheria na kanuni zinazoendesha Taasisi, Kuwa na viwango na vigezo vya kupima utendaji wa Menejimenti, kuelewa majukumu yake sawa sawa na wajumbe kujiepusha na kufanya kazi za Menejimenti, Ushirikiano, kuthaminiani, kusikilizana na upendo na Falsafa ya utendaji wa Bodi.
Prof. Mkumbo alimaliza kwa kueleza majukumu mengine muhimu yanayopaswa kusimamiwa na Bodi ambayo ni kutengeneza mikakati ya kufikia malengo ya chuo na kusimamia utekelezaji wake ikiwemo kutoa mpango wa upimaji wa matokeo, Kusimamia Menejimenti kutekeleza Mkataba wa utendaji (Perfomance Contract) na Kutoa changamoto kwa Menejimenti ya Chuo kuwa wabunifu katika kuanzisha vyanzo mbalimbali vya mapato.
Nae, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe aliutaka uongozi wa chuo kutoa elimu, ujuzi na kuwajengea wanafunzi uelewa na uwezo wa kuthubutu wa kufanya jambo wanalodhani ni muhimu ili wanapohitimu waamue kutafuta ajira au kujiajiri ili kuondokana na dhana ya kuwa Serikali haiwasaidii.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Eliuther Mwageni alitoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa ya kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi huku akiahidi kushirikiana na wajumbe wa bodi kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu ili kufikia dhima na malengo ya chuo hicho.