Habari
Rai yatolewa kwa wananchi kuutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kutunza na kuuza mazao yao
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imetoa rai kwa wananchi kuutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kutunza na kuuza mazao yao kwa bei shindani zilizopo sokoni ili kupata manufaa na kujenga uchumi kwa ujumla
Aidha, ametoa wito kwa Wananchi hao na kutoa ushirikiano ikiwemo kutoa taarifa kwa Viongozi wa Wilaya au Mkoa husika mara wanapoona watu wachache wenye nia ovu ya kudhoofisha Mfumo huo ili wachukuliwe hatua stahiki.
Hayo yamesemwa Oktoba 20, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Deodatus Mwanyika ( Mb) wakati ilipotembelea Mkoa wa Morogoro kujionea jinsi Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unavyowanufaisha wakulima katika zao la Kakao.
Vilevile, Mwenyekiti huyo ameielekeza Bodi ya Stakabadhi za Ghala (WRRB) kueneza Mfumo huo katika mikoa yote Nchini pamoja na kuongeza idadi ya mazao huku akiitaka kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu ili Mfumo huo uendelee kumnyanyua Mkulima.
Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe akijibu hoja mbalimbali amewaasa Wananchi hao kuendelee kufanya kazi kwa bidii na kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa manufaa yao na wawe wavumilivu kwa muda wa siku tatu hadi tano wakisubiri fedha zao baada ya kuuza mazao kupitia Mfumo huo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro
Mhe. Adam Malima amewashauri wakulima kuutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kuwa Mkoa wake umejipanga kuongeza uzalishaji wa mazao hususani zao la Karafuu na Chikichi ambapo kila kaya itapanda miche 40 ya karafuu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB Bw. Asangye Bangu amesema Bodi hiyo imepokea maelekezo ya Kamati hiyo na ameahidi kuwa itaendelea kuusimamia Mfumo huo ili kuhakikisha kuwa unawanufaisha wakulima wa mazao watakaoutumia.
Nao Wananchi wa Mvomero kata ya Turiani wakiongea na Kamati hiyo wamekiri kuwa Mfumo huo ni mzuri na wamefanikiwa kuuza Kakao kwa bei kutoka 2500 hadi tsh 29,000 kwa kilo mwaka 2024.