Habari
SERIKALI IMELENGA KUIMARISHA UWEZO WA WAFANYABIASHARA WADOGO NA KATI KUSHINDANA KATIKA MASOKO

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo ameeleza kuwa katika mpango wa Miaka mitano wa maendeleo ambao umepitishwa, Serikali imelenga kukuza na kurasimisha biashara ndogo ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao yanayozalishwa na wafanyabiashara wadogo na kati.
Prof. Mkumbo alieleza hayo Agosti 09, 2021 Dar es salaam katika uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa Uimarishaji wa Uwezo wa Wafanyabiashara wadogo na kati wa Kuboresha Ushindani katika Masoko ya Ndani, Kikanda na Kimataifa kwenye minyororo ya Thamani teuliwa ulioamabatana na hafla ya kukabidhi magari mawili kwa ajiri ya uratibu wa mradi huo.
Mradi huo unafadhiliwa na Enhanced Integrated Framework (EIF) pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa dola milioni 2.6 na utaimarisha uwezo wa Wafanyabiashara wadogo na kati kuboresha ushindani katika masoko ya ndani, kikanda, na kimataifa kwa miradi ya minyororo ya thamani iliyochaguliwa pia kuchangia katika kupunguza ukosefu wa ajira miongoni mwa wanawake na vijana.
Utekelezaji wa mradi huu utafanyika katika mikoa iliyochaguliwa ya Tanzania Bara na Zanzibar, ukilenga mikoa ifuatayo – Kigoma (Mafuta ya mawese), Mara na Simiyu (Kilimo cha mbogamboga), Singida (Asali), Kaskazini Pemba (Mwani) na Kaskazini Unguja (dagaa).
Naye Christine Musisi Muwakilishi Mkazi wa UNDP alisema dhamira yao ni kuendelea kushirikiana na serikali katika juhudi zake za kupunguza umaskini. Jitihada za kuimarisha Wafanyabiashara wadogo na kati zimekuja kwa wakati mzuri na tunafurahi kushirikiana na EIF kuwezesha Wizara zote mbili kutambua faida ya ushindani wa Tanzania kufungua uwezo wa juu wa sekta ya biashara iliyolenga katika Asali, Mafuta ya Mawese na Kilimo cha mbogambogaTanzania Bara, mwani na dagaa kwa upande wa visiwani Zanzibar