Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Exaud Kigahe (Mb) amesema Serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha uzingatiwaji wa viwango vya juu vya uzalishaji, hususan katika chuma, mabati na bidhaa za plastiki, ili kuwezesha bidhaa za Tanzania kushindana katika masoko ya kimataifa.
Mhe.Kigahe ameyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo walipotembelea kiwanda cha Lodhia kilichopo Mkuranga, mkoa wa Pwani ili kutathmini usimamizi wa viwanda vya ndani na kujadili hatua za kulinda wazalishaji wa ndani Februari 8, 2025.
“Katika kusisitiza hili Tumekuja na taasisi za udhibiti, zikiwemo Wakala wa Vipimo (WMA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili kuhakikisha viwanda vyetu vinalindwa dhidi ya ushindani usio wa haki na uingizwaji wa bidhaa duni,” amesema Kigahe.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge, Mhe. Deodatus Mwanyika, alisisitiza umuhimu wa kuongeza viwanda zaidi huku akisisitiza vilivyopo vilindwe ili viweze kuwa endelevu na vya faida.
“Moja ya mapendekezo yetu Makuu kwa Serikali ni kuongeza idadi ya viwanda na kuhakikisha kuna mazingira ya ushindani wa haki kwa wawekezaji. Tunazihimiza taasisi za udhibiti kuimarisha hatua za kudhibiti ubora wa bidhaa na kuwahamasisha Watanzania kupendelea bidhaa bora badala ya zile duni na za bei rahisi,” amesema Mwanyika.
Amesema kama biashara imeanza na kunakuwa na mabadiliko ya vitu ambavyo havikuwapo wakati uwekezaji unafanyika ikiwemo kuruhusu kampuni za nje kuvamia soko inaweza kuwa na athari.
Hali hii imefanya zaidi ya tani 3500 za bati zinazozalishwa na kiwanda hiki kutokwenda sokoni kwa sababu ya kutokuwapo kwa usawa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Lodhia Industries na Mmiliki, Arun Lodhia alieleza changamoto wanazokabiliana ikiwemo kutotosheleza kwa umeme.
Pia aliitaka serikali kuweka adhabu kali kwa wazalishaji wanaovunja viwango vya ubora, akipendekeza kuwa faini zianzie Sh100 bilioni au viwanda husika vifungiwe.
Pia alitaka miradi ya ndani inayotekelezwa kutoa kipaumbele kwa bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuchochea ukuaji wa viwanda