Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali itahakikisha bidhaa za ndani zinapata soko kubwa ndani na nje ya nchi.


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo(Mb) amesema kama Serikali itahakikisha bidhaa za ndani zinapata soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Ameyasema hayo Oktoba 28,2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake katika Kiwanda cha kuzalisha mabati ALAF alipokwenda kutembelea kuona upanuzi wa kiwanda hicho hasa kwenye uzalishaji wa mabati ya rangi unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Dkt.Jafo amesema kwa sasa uzalishaji wa bidhaa za bati umekuwa mkubwa ukilinganisha na mahitaji ya bidhaa hizo,hivyo serikali inaangalia namna ya kuzuia bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi ambazo zinatengenezwa kwa wingi nchini ili kuongeza ajira kwa Watanzania na kusaidia bidhaa hizo kupata soko.

Aidha Dkt.Jafo amesema uwepo wa uwekezaji wa Viwanda hivyo ni uthibitisho tosha kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan inapiga hatua kubwa katika uwekezaji wa Viwanda Nchini.

Nae Meneja Masoko wa ALAF Bi.Isamba Kasaka amesema upanuzi wa kiwanda hicho cha kutengeneza mabati ya rangi utasaidia upatikanaji wa mabati hayo kwa wingi na kwa ubora wa hali ya juu.

Vilevile amesema upanuzi wa kiwanda hicho utaongeza ajira kwa Watanzania pamoja na ongezeko la ulipaji kodi kwa Serikali.