Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji katika Sekta ya Viwanda na Biashara


Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji katika Sekta ya Viwanda na Biashara kwa lengo la kuwavutia wawekezaji nchini Tanzania na kutengeneza ajira pamoja na kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) alipotembelea kiwanda cha Lodhia kinachotengeneza mabati kilichopo Kisanvule, Mkuranga kwa lengo la kuona shughuli zinazofanywa kiwandani hapo Oktoba 8, 2024.

Waziri Jafo amesema kuwa ili kiwanda kiweze kuzalisha kwa faida kinatakiwa kuwa na umeme wa kutosheleza mahitaji ya Kiwanda.

Hivyo, Mhe. Jafo amemuagiza Mkurugenzi wa Shirika la Umeme - Tanesco kuweka transfoma ndani ya wiki tatu kuanzia leo ili kuhakikisha dhamira ya Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan ya kuwa na viwanda inakamilika.

Amesema kuwa kiwanda hicho kimetumia zaidi ya Shilingi bilioni 162 kufunga mitambo na hivyo wanapaswa kuanza uzalishaji.

“Huo ni uwekezaji mkubwa ambao utaongeza ajira nchini na pato la Taifa kwa ujumla. Uwekezaji umeendela kujipambanua na umeongeza wigo wa kupunguza tatizo la ajira.

“Nimeona baadhi ya changamoto ambayo Serikali ikiweza kufanyia kazi viwanda hivi vitafanya uzallishaji na hiki kiwanda kipya kabisa kadhalika kitaanza uzalishaji.

Alisema tatizo la trasfoma tayari Mamlaka ya Mapato Tanzania imeshakamilisha taratibu hivyo ni jukumu la Tanesco kulifanyia kazi ili umeme uwafikie wawekezaji wa Mkuranga.

Naye Mkurugenzi wa Kiwanda cha Lodhia, Sailesh Pandit alisema kwa sasa Kiwanda kimekamilika na wanasubiri kupata umeme ili waanze uzalishaji.

Pandit alisema uzalishaji utakapoanza wanatarajia kuzalisha kati ya tani 5000 hadi 10000 kwa mwezi.
Alitoa rai kwa watanzania kusupport viwanda vya ndani hivyo waondoe kasumba ya kupenda bidhaa za nje badala yake waone fahari kununua bidhaa inayotengezwa nchi.
“Watanzania tunatakiwa kusaidiana na kuona fahari ya kununua bidhaa wanayoiona inavyotengezwa nchini kwao. Kuna kasumba fulani yakuona bidhaa za nje ni bora kuliko za ndani. Lakini niwahakikishie bidhaa zetu zinakidhi ubora wa kimataifa.

“ Baada ya wiki tatu tunaanza uzalishaji wa mabati kama ambavyo waziri amesema TRA wamekamilisha na kuruhusu transforma itolewe bandarini.