Habari
Serikali kuendelea kuongeza ajira kwa Vijana kwa kuboresha mazingira ya kujiajiri na kuajiriwa.
Serikali kuendelea kuongeza ajira kwa Vijana kwa kuboresha mazingira ya kujiajiri na kuajiriwa.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb), amekipongeza Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa ubunifu wake hususan kwa kuboresha mitaala yake na kufanya mpango wa uanagenzi pamoja na atamizi za biashara.
Mhe. Kigahe ameyasema hayo kwenye Mahari ya 59 ya CBE kwa Kampasi Kuu Dar es salaam yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (JNICC), leo Novemba 08, 2024.
Amesema kuwa Serikali inathamini mchango wa CBE katika kuzalisha wataalamu na inaunga mkono juhudi za kuboresha mitaala ili kuzalisha wataalamu na kwamba Taifa linahitaji wataalamu wenye uzoefu kwa vitendo na uwezo wa kujiajiri na kuajiri wenzao.
“Nimefurahishwa sana na juhudi za CBE, kupitia mpango wa uanagenzi na atamizi za biashara kwani zinaendana na mpango wa Serikali wa kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wetu na nimpango ambao Taifa letu unauhitaji kwa sasa, katika kuwaandaa vijana wetu kuingia kwenye soko la ajira wakiwa na uzoefu kwa vitendo na kujenga uwezo wa kujitegemea,”alisema Mhe. Kigahe.
Hata hivyo, Mhe. Kigahe ametoa wito kwa makampuni ya ndani na Taasisi nchini kuendelea kushirikiana na Chuo cha CBE katika kuwawezesha wanafunzi kupata uzoefu kwa vitendo.
Aidha, Sekta ya Viwanda na Biashara ni tegemeo la uchumi kwa nchi yoyote kwani ndiyo chanzo cha ajira za uhakika.
Hata hivyo amelipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC), mabenki na wenye viwanda kwa kuendelea kuajiri vijana wengi waliohitimu masomo yao katika Chuo cha CBE.