Habari
Serikali kuunganisha Leseni za Biashara zinazotolewa na BRELA na Halmashauri kuwa moja

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amesema Serikali iko mbioni kuunganisha leseni ya biashara inayotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Halmashauri kuwa leseni moja ya biashara itakayowawezesha kufanya biashara Nchi nzima.
Dkt Kijaji ameyasema hayo Agosti 17, 2023 wakati akijadiliana kuhusu maendeleo ya biashara na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma katika Ukumbi wa Ofisi za Mkuu wa Mkoa ikiwa ni mwendelezo wa mikutano hiyo katika kila mkoa ambapo Dodoma ni Mkoa wa Saba baada ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Morogoro Mbeya na Songwe.
Aidha, Dkt. Kijaji amewashauri wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma kusajiri biashara zao, kuwa waaminifu katika kurudisha mikopo na kuchangamkia fursa za biashara kwa kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi pamoja na fursa za kibiashara katika masoko ya EAC, SADC, AGOA na AfCFTA yenye soko lenye jumla ya watu bilioni 1.3. bila kutozwa kodi wala ushuru wowote.
Dkt. Kijaji pia amesema Wizara yake inaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini (MKUMBI) ambapo hadi sasa imefuta au kupunguza Tozo, Ada na Faini 374 kati ya 380 na katika kipindi cha 2023/24 Tozo, Ada na Faini 67zimefutwa au kupunguzwa.
Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Exaud Kigahe akijibu Baadhi ya changamoto za wafanyabiashara hao amesema Serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi na itaendelea kuishirikisha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini pamoja na jitihada za uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini.
Kwa upande wa Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe Fransis Mtinga aliwahakikishia wafanyabiashara hao kuwa Kamati hiyo iko tayari kushughulikia changamoto zote za kisheria na sheria ndogo zinazowakabili katika ufanyaji biashara.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi Rosemary Senyamule amemhakikishia Waziri Kijaji kuwa Mkoa wake kwa kishirikiana na wadau mbalimbali utashughulikia changamoto zote ziliowasilishwa na wafanyabiaahara hao ikiwemo utoaji wa mafunzo kwa wajasiliamali na kuanzisha kituo cha huduma za pamoja za kuhudumia wafanyabiashara.
Awali Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Dodoma Bw Hamis Fungameza pamoja na wafanyabiashara wengine walipata fursa za kuwasilisha changamoto mbalimbali ikkwemo upatikanaji wa Mitaji, Mikopo yenye masharti magumu, masoko ya mazao, kodi ambazo si rafiki , miundombonu ya barabara na masoko hafifu