Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali ya Tanzania Yakaribisha Wawekezaji kutoka UAE


Serikali ya Tanzania Yakaribisha Wawekezaji kutoka UAE

Serikali ya Tanzania imewakaribisha Wawekezaji kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuja kuwekeza nchini, hususan katika mji wa Dar es Salaam, ulioandaliwa kuwa miongoni mwa miji mikuu itakayohudumia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb), wakati akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na UAE lililoratibiwa na TANTRADE, TIC, TCCIA na Chemba ya Biashara ya Dubai na kufanyika Disemba 12, 2024 katika ukumbi wa Johari Rotana Jijini Dar es salaam.

Aidha, Waziri Jafo amefafanua kuwa Wawekezaji hao wanakaribishwa kuwekeza katika kuwekeza katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, uzalishaji, madini, utalii, na miundombinu mbalimbali ikiwemo hoteli za kifahari, viwanja vya michezo, na uwanja wa ndege wa kimataifa.

Vilevile amebainisha kuwa Tanzania ambayo ni lango la Afrika Mashariki na Kusini, kutokana na eneo lake la kijiografia na miundombinu yake inaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi kwa Wawekezaji na Wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kurahisisha taratibu za biashara na kutoa msaada wa kiufundi ilinkuvutio wawekezaji.

"UAE ni mshirika muhimu wa maendeleo kwa Tanzania. Tunathamini sana uhusiano wetu wa kiuchumi na kijamii na tunatarajia kuimarisha ushirikiano wetu zaidi wa kibiashara. Kwa mfano, mwaka 2022, Tanzania ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 1.07 kwenda UAE, wakati UAE ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 2.48 kwenda Tanzania.," alisema Dkt. Jafo.

Naye Balozi wa UAE nchini Mhe. Khalifa Abdulrahman Almarzooqi pamoja na Balozi wa Tanzania nchini UAE Mhe. luteni Jenerali Yacoub Hassan Mohamed wamesema Nchi hizo mbili zitaendelea kuimarisha uhusiano wake wa kihistoria na wa kibiashara ili kuendelea kukuza uchumi na kuleta maendeleo baina ya nchi hizo na wanachi wake kwa ujumla .