Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Stakabadhi za Ghala, umeendelea kuwa chombo muhimu katika kuimarisha urasimishaji wa biashara


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Dkt.Selemani Jafo (Mb) amesema mfumo wa Stakabadhi za Ghala, umeendelea kuwa chombo muhimu katika kuimarisha urasimishaji wa biashara ya mazao kwa kuweka uwazi, kuongeza ushindani wa bei na kuwahakikishia wakulima masoko ya uhakika.

Dkt.Jafo ameyasema hayo Februari 7,2025 jijini Dodoma  wakati akizungumza na waandishi wa habari , kuhusu kuhitimisha msimu wa biashara ya bidhaa za kilimo kupitia mfumo huo kwa Mwaka 2024/2025 na kujiandaa na msimu mpya wa 2025/2026.

Amesema kuwa, wadau hao ni pamoja na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Soko la Bidhaa Tanzania, TAMISEMI, Sekta Binafsi, Taasisi za Fedha pamoja na Mamlaka ya Biashara Tanzania.

“Tumeshuhudia ongezeko la mazao yanayouzwa kupitia mfumo huu, ongezeko la ghala zilizosajiliwa na ushiriki mkubwa wa wakulima katika kuuza mazao yao kwa utaratibu rasmi,”amesema Dkt.Jafo

Aidha, amesema  katika msimu wa 2024/2025, jumla ya bidhaa 14 zilikusanywa na kuuzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, zikiwemo Chai, Choroko, Dengu, Kahawa, Kakao, Korosho, Maharage, Mahindi, Mbaazi, Mchele, Mihogo, Mpunga, Soya, na Ufuta.

Hata hivyo ameeleza kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya mfumo huo, wameshuhudia ongezeko kubwa la uzalishaji na ukusanyaji wa mazao, ambapo jumla ya kilogramu 810,230,588 zilikusanywa, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 80 ikilinganishwa na msimu wa 2023/2024, ambapo kilogramu 451,192,592 zilikusanywa.

Amesema kuwa ongezeko hilo halikuakisiwa tu katika kiwango cha mazao bali pia katika thamani ya mapato ya wakulima.

“Kutokana na wingi wa bidhaa pamoja na kuimarika kwa bei sokoni, wakulima walilipwa jumla ya Sh.Trilioni 2.9, ongezeko la asilimia 142 ikilinganishwa na Sh.Trilioni 1.2 walizopata msimu uliotangulia,”amesema

Waziri Jafo, amesema hali hiyo ni uthibitisho wa jinsi mfumo wa stakabadhi za ghala unavyoendelea kuwa chombo madhubuti cha kuhakikisha wakulima wananufaika ipasavyo na jasho lao.