Habari
ACCURATE MARKET GEOGRAPHIC DATA IS THE PILLAR OF THE ECONOMY
Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa matumizi ya taarifa sahihi na za kijiografia za masoko (Market Intelligence) ndiyo nguzo kuu itakayoiwezesha nchi kufanya mapinduzi ya kiuchumi kupitia sekta ya biashara na kilimo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb.), alipokuwa akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb.) katika Mkutano wa Ngazi ya Juu uliowekwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) uliolenga kujadili mbinu za kuongeza ushindani wa sekta ya kilimo na chakula nchini katika Viwanja vya nanenane Nzuguni-Dodoma Agosti 07,2026.
Londo amesema kuna umuhimu wa matumizi ya maarifa na taarifa sahihi katika kuongeza tija kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, na wafanyabiashara kufanya maamuzi sahihi kuhusu aina ya mazao, muda wa uzalishaji, na maeneo yenye fursa za kibiashara ili kutoa matokeo yenye tija katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050.
Londo amebainisha kuwa mfumo wa uzalishaji nchini lazima ubadilike kutoka kuzalisha kwasababu tu ya uwepo wa ardhi na hali ya hewa, na badala yake uelekee kwenye uzalishaji unaoongozwa na mahitaji halisi ya masoko.
Aidha ameeleza kuwa utekelezaji wa Dira mpya ya maendeleo unajikita katika kubadilisha mtazamo wa uzalishaji kwa kutumia maarifa ili kuongeza thamani ya mazao na kujenga uchumi wa viwanda.
Amebainisha kuwa sekta za uzalishaji ni nguzo kuu katika biashara, hivyo lengo kuu ni kuhakikisha malighafi zinazotokana na kilimo, mifugo na uvuvi zinaongezewa thamani hapa nchini badala ya kuuzwa bila kuchakatwa na huku ikilenga kubadili changamoto zilizopo kuwa fursa za kibiashara na kiuchumi.
Londo amesisitiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na maelekezo ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), kuwa ni kuhakikisha bidhaa zote za kibiashara zinazalishwa kwa viwango vinavyokidhi masoko huku akibainisha kuwa Wizara imejipanga kufungua na kuimarisha fursa za masoko ya ndani, kikanda na kimataifa ili kutoa uhakika wa soko kwa wazalishaji wa Kitanzania.
