Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Taasisi wezeshi katika sekta ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji Nchini kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Selemani Jafo ametoa rai kwa wawekezaji Nchini kuendelea kuwekeza na kufanya upanuzi wa viwanda vyao ili kuongeza uchumi wa Nchi ili kutatua tatizo la ajira nchini na kuzalisha bidhaa bora kwa kutumia malighafi zinazopatikana Nchini.

Ameyasema hapo wakati anafunga Maonesho ya pili Kimataifa ya Viwanda Tanzania (TIMEXPO-2024) yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwl. Julius Nyerere (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam, Oktoba 02,2024.

Dkt.Jafo amesema kwa kuzalisha bidhaa bora kwa wingi Nchini kutasaidia kuondokana na tabia ya kuwa wachuuzi na badala yake Taifa litakuwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa zake kutoka nchini kwani Serikali imajipanga kuongeza maeneo ya uwekezaji wa viwanda katika Mikoa yote nchini na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Aidha Mhe.Jafo ameziagiza Taasisi wezeshi katika sekta ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji Nchini kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji wa Viwanda na Biashara badala yake kuwa wawezeshaji katika sekta hiyo kwani ndio matarajio ya Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kuona sekta hiyo inasonga mbele.

Aidha Dk.Jafo ametoa rai kwa wananchi kujali na kutumia zaidi bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuhamasisha uwekezaji na kivifanya Viwanda vya Tanzania kusonga mbele.

Vilevile amesema ni Imani yake kuwa kwa kijana yeyote aliyeshiriki kikamilifu katika Maonesho hayo atakuwa majefunza mengi zaidi na kuagiza vyuo vitangaziwe ili viweze kutoa vijana wengi waweze kujifunza.

Maonesho hayo ya pili ya Kimataifa ya Viwanda (TIMEXPO 2024) ambayo yamefunguliwa rasmi na Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dkt.Doto Biteko Septemba 26,2024 yamefungwa rasmi hii leo Oktoba 2,2024.