Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Tafiti ni Msingi wa Ukuaji wa Biashara na Uchumi


Tafiti ni Msingi wa Ukuaji wa Biashara na Uchumi
Waziri wa Biashara na Viwanda Mhe Dkt. Selemani Jafo (Mb) amesema Serikali inaweka mazingira bora ya ufanyaji biashara kwa wadau wote, kushirikiana na Sekta Binafsi na Washirika wa Maendeleo na kuendelea kurekebisha Sera na Sheria zinazolenga kujenga uchumi imara dhidi mabadiliko.

Vilevile amesisitiza matumizi ya tafiti zinazofanywa na Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini nchini (REPOA) katika kuimarisha ukuaji wa biashara katika kukidhi ushindani wa kimataifa katika soko, uchumi, na maisha ya wananchi ili kufikia malengo ya Sera zitakazosaidia Nchi za Afrika katika maendeleo ya uchumi endelevu.

Ameyasema hayo kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dotto Biteko Oktoba 29, 2024 jijini Arusha alipokuwa akifungua Warsha ya 28 ya Utafiti ya Mwaka ya REPOA (ARW) 2024 inayofanyika Oktoba 29 - 30, 2024 jijini Arusha.

Aidha Dkt. Jafo ametoa wito kwa REPOA na Washirika wake kuendelea kuimarisha ushirikiano na sekta za umma na binafsi pamoja na kuongeza uelewa kuhusu fursa za biashara zinazotolewa na Mikataba ya AfCFTA) na Tripartite ya EAC, SADC na COMESA.

Naye Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Shaban Omary amesema Serikali zote mbili za JMT na SMZ zimekuwa zikitumia taarifa za utafiti kutengenezea Sera, Sheria pamoja na Mipango mbalimbali ya maendeleo na ni wajibu wa Watanzania kujifunza kutumia tafiti katika kufanya maamuzi na kuwa tayari kwa mabadiliko.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dkt. Donald Mmari amesema Warsha hiyo inalenga kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili Afrika pamoja na kuangalia jinsi fursa za AFCFTA zinavyoweza kukuza biashara, uzalishaji wenye tija, mahusiano ya kibiashara, minyororo ya thamani na ugavi kukuza uchumi wa Afrika kwa ujumla.
.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Maua, Matunda na Mbogamboga (TAHA) Bi Jacqueline Mkindi amesema warsha hiyo itasaidia kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kuainisha fursa zilizopo katika ikiwemo changamoto ya usafirishaji wa mazao hayo kwa kutumia njia rahisi, gharama nafuu na kwa haraka