Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TAMISEMI YAUNGA MKONO BUNIFU ZA TEMDO


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw Adolf Ndunguru amesema TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) kwa kuzihamasisha Halmashauri zote nchini kuanza kutumia bidhaa na vifaa tiba vinavyozalishwa na Shirika hilo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan kwenye sekta za afya, elimu na kilimo.

Ameyasema hayo Oktoba 19, 2025 alipotembelea Taasisi hiyo na kujionea jinsi bidhaa hizo zinavyozalishwa na jinsi Taasisi zilizo chini ya TAMISEMI zinavyoweza kushirikiana na TEMDO katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na ya kimkakati.

Aidha, amebainisha kuwa katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, Serikali itaendelea kuhakikisha sekta ya afya inaimarika ukiwa ni pamoja na kutumia vifaa tiba bora vinavyopatikana kwa gharama nafuu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.

Bw. Ndunguru pia, aliisisitiza TEMDO kuendeleza ubunifu zaidi katika bidhaa inazozitengeneza ili ziweze kuhimili ushindani wa soko na kutumiwa na hospitali pamoja na vituo vya afya mbalimbali nchini

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah ameihakikishia TAMISEMI kuwa TEMDO ina uwezo wa kutengeneza vifaa tiba kwa viwango vya kimataifa vilivyothibitishwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) pamoja na Bohari ya Dawa (MSD) na kuwa iko tayari kutoa huduma kwa Halmashauri zote nchini.

Naye, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TEMDO Profesa Lazaro Busagala amebainisha kuwa TEMDO inazalisha bidhaa zaidi ya 16 ikiwemo vifaa tiba vya hospitali kama majokofu ya kuhifadhia maiti, vichomea taka hatarishi na vitanda vya aina mbalimbali vinavyohitaji soko la ndani.

Awali akitoa taarifa kwa Makatibu Wakuu hao huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa TEMDO, Profesa Frederick Kahimba amebainisha kuwa kuanzia mwaka 2022 hadi sasa Taasisi imetengeneza vifaa tiba zaidi ya
1,000, vyenye thamani zaidi ya zaidi ya bilioni mbili na wateja wake ni MSD, Bugando, Uhuru Hospital, na Hospitali za Kanda za Wizara ya Ulinzi, JKT, Jeshi la Polisi, Hospitali ya Wilaya ya Maswa na Jiji la Arusha (CSR).