Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANTRADE NA SHIRIKA LA POSTA WATIA SAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO WA BIASHARA MTANDAO - POSTA ONLINE SHOP


Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na Shirika la Posta watia Saini Makubaliano ya ushirikiano wa Biashara – Mtandaoni “Posta online shop”

 

Ushirikiano huu unalenga kuhamasisha wafanyabiashara, wenye viwanda na wajasiriamali kutumia duka hilo ili kupata masoko ya ndani na kimataifa na kuongeza mauzo, mfanyabiashara na mteja kuuza, kununua na kutangaza bidhaa kimtandao.

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) wakati akizindua mashirikiano ya kibiashara ya Shirika la Posta Tanzania na TANTRADE amewapongeza kwa maono hayo kwa kuchukua hatua za kutumia maendeleo ya teknolojia kuwaunganisha wafanyabiashara eneo moja na kuwatambulisha katika soko la ndani na nje ya Nchi.

 

 

“niwapongeze Posta kwa kuanzisha na kumiliki duka mtandaoni “Posta online shop” na kuwa na uelewa wa kufanya kazi za duka hilo huku ikishirikiana na TANTRADE katika kulitambulisha duka hilo kwa Watanzania ili lipanue wigo wa kuhudumia jamii pana ya watanzania na watu wote ulimwenguni.” amesema Dkt. Faustine Ndugulile

 

Aidha, Dkt. Faustine Ndugulile ameongeza kuwa duka hili ni mojawapo ya maduka yanayowakusanya wafanyabiashara na wanunuzi tofauti tofauti kwa pamoja (Multivendor market platform) kama Viwanda, wafanyabiashara na wajasiliamali wadogo na wa kati wakiwa wanufaika wakuu wa duka hili la mtandao, huku likitoa uhakika wa kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi na kuwafikia wateja popote walipo kwa wakati na kwa usalama.

 

Dkt. Faustine Ndugulile ameongeza kuwa Serikali ilianzisha Wizara yake mpya ikiwa na mikakati ya kukuza matumizi ya Tehama katika kuwahudumia wananchi kwa lengo la kuwapunguzia muda wa kupata huduma sambamba na gharama, kwa sasa mkakati wa nchi ni kuelekea kwenye uchumi wa kidigitali ‘Digital Economy’ hivyo nyinyi kati ya Mashirika ya umma mnatakiwa kuwa mstari wa mbele kupokea na kutekeleza mabadiliko haya kwa manufaa ya taifa na jamii ya watanzania kwa ujumla.

 

Nae, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amezitaka taasisi hizo mbili za Shirika la Posta Tanzania na TANTRADE Kujidhatiti zaidi kwenye kukabiliana na ushindani wa kibishara pia kutumia ukuaji wa teknolojia kama fursa ya kukuza uchumi wa nchi na kujipambanua kibiashara kwa kutafuta soko na kuitumia kurahisisha utendaji kazi na kutoa fursa ya wafanyabaishara mbalimbali kukuza biashara zao kupitia mitandao ya kijamii kwani kwa sasa dunia iko mahali pote kupitia simu janja

 

Hafla hiyo imefanyika leo 07Julai, 2021 kwenye viwanja vya Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam - DITF (Saba saba) na kuhudhuliwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb), Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari  Dkt. Zainab Chaula, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade na Balozi Mteule Bw. Edwin Rutageruka, Kaimu Postamasta Mkuu Shirika la Posta Tanzania Bw. Bwana Macrice Mbodo, Wakuu wa Taasisi Mbalimbali na wadau