Habari
TANZANIA NA KENYA ZAAHIDI KUENDELEA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA

TANZANIA NA KENYA ZAAHIDI KUENDELEA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA.
Serikali ya Tanzania imeahidi kuendelea kuondoa changamoto za biashara zisizokuwa za kiushuru baina ya Tanzania na Kenya na kugeuza vikwazo hivyo kuwa fursa mbalimbali za biashara ili kuimarisha uhusiano ulipo baina ya nchi hizo.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt Hashil Abdallah Oktoba 1, 2025 wakati akifungua Mkutano Mkutano wa Tisa (9) wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya Tanzania na Kenya unaofanyika Dar es Salaam nchini Tanzania ukiwa na lengo la kuondoa vikwazo visivyo vya kiushuru na changamoto za biashara zilizopo baina ya nchi hizo.
Aidha, amebainisha kuwa biashara ndio msingi wa uhusiano baina ya nch hizo ikilenga kuboresha maisha ya wananchi wa pande zote mbili kwa kuongeza ajira, kujenga viwanda na kuhamasisha ubunifu wa wajasiriamali katika nyanja mbalimbali zenye kuleta Maendeleo
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya, Bi. Regina A. Ombam amesema Tanzania na Kenya zina ushirikiano wa kihistoria, tamaduni na uchumi ambapo uchumi wa Tanzania unaendelea kuonyesha uthabiti mkubwa, unaoendelea kukua hususani katika na sekta ya viwanda, ujenzi na utalii huku ukifungua fursa kubwa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Kenya.
Amesema Kenya imeendelea kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji yanayowanufaisha wananchi wa Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania.
“Sisi si majirani tu, bali ni mataifa ya kindugu, yaliyofungwa na dira ya pamoja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye ustawi, mshikamano na amani,” amesema.