Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANZANIA NA ZAMBIA WAAZIMIA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA


Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zambia zimeazimia kuendelea kuchukua hatua katika kuondoa vikwazo vya biashara ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, huduma na watu, hatua inayolenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika Mkutano wa 5 wa Kamati ya Pamoja ya Biashara (Joint Trade Committee – JTC) kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika leo, Mei 7, 2026, mjini Tunduma. Mkutano huo uliwakutanisha Mawaziri na viongozi waandamizi kutoka sekta mbalimbali kwa lengo kupitia utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano uliopita na kujadili masuala mapya ya kibiashara.

Akizungumzia kuhusu mkutano huo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Judith Kapinga (Mb) ameeleza kuwa wamejadili changamoto mbalimbali za biashara baina ya pande zote mbili zipatazo 20 na kufanikiwa kutatua changamoto 7, huku pande zote zikiwekeana mipango ya muda mrefu na mfupi ya kushughulikia changamoto za biashara 13 zilizosalia.

Naibu Waziri Londo amezitaja changamoto hizo zilizotatuliwa kuwa ni;- ulinganifu wa viwango vya upimaji mafuta kupitia Makubaliano ya Mkataba wa Kutambua Matokeo ya Vipimo kati ya Mamlaka zinazohusika na Vipimo, ili kuhakikisha ufanisi na uaminifu wa mchakato wa upimaji mafuta; Kuondolewa kwa marufuku ya usafiri wa usiku nchini Zambia, hatua inayowezesha magari ya mizigo kusafiri saa 24 na hivyo kuongeza ufanisi wa usafirishaji na mtiririko wa biashara; na Maboresho ya usimamizi na uchakataji wa nyaraka za mizigo kupitia utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mfumo wa kubadilishana taarifa za forodha na kuanza kwa awamu ya pili ya uwianishaji wa mifumo.

Zingine ni;- Kuondolewa kwa ada ya vibali vya usafiri ya Kwacha 4,500 kwa wasafirishaji wa Tanzania, hatua inayopunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ushindani; Kuondolewa kwa ada ya vibali vya biashara visivyo vya usawa ya USD 200 kwa wasafirishaji wa Zambia wanaoingia Tanzania, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama na kuongeza ufanisi wa biashara; na Kutatuliwa kwa suala la kushikiliwa kwa pasipoti za madereva.