Habari
TANZANIA YAUZA BIDHAA ZA TAKRIBANI DOLA MILIONI 22 NCHINI SAUDI ARABIA ASEMA LONDO
📌ni kupitia ushirikiano wa kibiashara baina ya pande hizi mbili;
📌Naibu Waziri Londo ashiriki maadhimisho ya miaka 96 ya Taifa la Saudi Arabia kama mgeni rasmi;
📌Balozi wa falme ya Saudi Arabia ampongeza Mhe Rais kwa kudumisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Na. Neema Chalila Mbuja
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dennis Londo amesema Tanzania imefanikiwa kuuza bidhaa za takribani dola milioni 22 nchini Saudi Arabia kutokana na ushirikiano wa kibiashara uliipo kati ya Tanzania na Saudi Arabia.
Mhe Londo ameyasema hayo wakati wa hafla ya kusherehekea miaka 96 ya Taifa la Saudi Arabia ambapo alikuwa mgeni rasmi , hafla iliyohudhuriwa na mabalozi na wawakilishi mbalimbali wa makampuni ya kimataifa.
Amesema Tanzania na Saudi Arabia zinaendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria na ushirikiano katika sekta mbalimbali, ikiwemo biashara, elimu na uwekezaji na kuongeza kuwa uhusiano huo umeendelea kuimarika, huku wigo wa biashara ukiongezeka na Watanzania wengi wakipata fursa za ufadhili wa masomo (scholarships) nchini Saudi Arabia.
Londo amesema Tanzania imekuwa ikiagiza mafuta, bidhaa za petrochemical na mbolea kutoka Saudi Arabia, huku Saudi Arabia ikiagiza nyama na bidhaa za kilimo kutoka Tanzania.
Kwa upande wake Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Mhe yahya bin Ahmed Okaish amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kudumisha undugu, urafiki kati ya Tanzania na Saudi Arabia na kufungua milango ya biashara baina ya pande mbili.
