Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Tanzania zimefanikiwa kuuza bidhaa katika nchi mbalimbali tangu kuanza kwa Soko Huru la Afrika (AfCTA


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Exaud Kigahe (Mb) amesema kampuni 11 za Tanzania zimefanikiwa kuuza bidhaa katika nchi mbalimbali tangu kuanza kwa Soko Huru la Afrika (AfCTA).

Mhe.Kigahe ameyasema hayo leo Machi 3,2025 jijini Dar es Salaam wakati akizindua mpango wa uunganishaji wafanyabiashara wadogo na fursa za Soko Huru la Afrika unaotekelezwa kwa ushirikiano na CRDB Bank Foundation na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP).

Amesema kuwa bidhaa zilizouzwa kwa wingi ni nyuzi za katani tani 426.4, kahawa tani 275.3 na tumbaku tani 21.1 ambazo zimeuzwa kwenye nchi za Nigeria, Ghana, Morocco, Misri na Algeria.

Aidha, amesema kupitia programu hiyo washiriki watapata maarifa ya kipekee yatakayowawezesha kuchangamkia fursa katika soko hilo na tayari kamati ya kitaifa imeundwa kwa lengo la kutekeleza mpango huo.

Mhe. Kigahe ameipongeza Benki ya CRDB kupitia taasisi yake ya CRDB Bank Foundation kwa kuwa wanawake na vijana wanaunda zaidi ya asilimia 75 ya watu waliopo nchini na kuzitaka kampuni zingine kuiga juhudi hizo ili Watanzania wengi zaidi wanufaike na fursa za soko hilo.

Naye Mkurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema mchakato wa kuwatambua na kuainisha wajasiriamali watakaoshiriki katika programu hiyo tayari ulishafanyika katika mikoa 18 na zaidi ya wanawake wajasiriamali 600 wamechaguliwa na kuanza kupatiwa mafunzo.

Uunganishaji wa wajasiriamali na fursa za Soko Huru la Afrika ni sehemu ya mkakati wa Serikali na CRDB wa kukuza ujumuishi wa kiuchumi kupitia programu ya 'Imbeju'.

CRDB Bank Foundation ina jukumu la kuwajengea uwezo wajasiriamali kwa kuwapa elimu ya fedha, mafunzo ya usimamizi na uendeshaji wa biashara pamoja na kuwapatia mitaji wezeshi itakayowezesha kunufaisha na fursa za AfCTA," amesema Mwambapa.

Utekelezaji wa Mkataba wa Soko Huru la Afrika ulianza Januari 2021 na Bunge liliridhia Septemba 2021 na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yaliyokidhi vigezo vya kushiriki katika soko hilo lenye watu zaidi ya bilioni 1.5.